Home Habari Kuu Serikali kuandaa ibada ya wafu kwa waliokufa maji Maai Mahiu

Serikali kuandaa ibada ya wafu kwa waliokufa maji Maai Mahiu

0

Serikali kwa ushirikiano na makanisa, viongozi na watu wa Maai Mahiu itaandaa ibada ya wafu kwa ajili ya watu ambao walikufa maji katika eneo la Maai Mahiu.

Haya yalitangazwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua jana katika kanisa la ACK St. Marks New Kamiti, katika eneo bunge la Kiambu mjini, kaunti ya Kiambu ambako alihudhuria ibada.

Kiongozi huyo alizungumza pia kuhusu shughuli inayoongozwa na jeshi la KDF ya kutafuta miili ya wengine ambayo huenda imekwama kwenye tope.

Gachagua alitahadharisha wakenya dhidi ya kupita kwenye maeneo yaliyofurika kwani ni hatari.

Jumatatu Aprili 29, 2024, wakazi wa eneo la mji wa kale wa Kijabe na maeneo ya karibu waliamshwa na mshindo mkubwa wa maji yaliyokuwa yakiteremka kwa kasi sana.

Maji hayo mengi na yaliyokuwa na takataka nyingi yalisomba nyumba kadhaa na watu waliokuwa wamelala wasijue hatari iliyokuwa imewafika.

Baadaye ilibainika kwamba maji hayo yalikuwa yamejikusanya kwenye handaki moja karibu na reli huko Kinale kufuatia mvua nyingi iliyokuwa imenyesha kwa siku kadhaa.

Takataka ambayo ilikuwa kwenye handaki hilo ndiyo ilisababisha mkusanyiko huo wa maji na iliposukumwa ghafla maji hayo yakatiririka na kuathiri watu wengi.

Kufikia sasa idadi ya vifo kutokana na mkasa huo ni 58, idadi ambayo huenda ikabadilika kwani bado kuna watu ambao hawajulikani waliko na shughuli za utafutaji zinaendelea.

Website | + posts