Kenya itashirikiana na sekta ya kibinafsi ili kukuza uchumi wa kidijitali wa nchi, Rais William Ruto amesema.
Rais Ruto alisema Serikali imefanya uamuzi wa kimakusudi wa kutumia teknolojia ili kustawisha sera, programu na ajenda yake katika kuharakisha maendeleo.
Alitaja hatua hiyo ya kuhakikisha huduma zote za Serikali zinahamishiwa kwenye mfumo wa kidijitali kama kielelezo tosha kuwa teknolojia sasa inastawisha uchumi wa nchi.
Akizungumza wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 10 ya Maabara ya Utafiti-Afrika ya IBM katika Chuo Kikuu cha Katoliki cha Afrika Mashariki mtaani Karen siku ya Alhamisi, Rais alisema Wakenya sasa wanaweza kupata huduma 10,000 mtandaoni.
“Tuna nia ya kuhakikisha kuwa huduma zetu zote za Serikali zinasogezwa kwenye mfumo wa kidijitali kwa ufanisi,” alisema Rais Ruto.
Alisema mfumo wa kidijitali utahakikisha ufanisi hivyo kuondoa uzembe, ufisadi na ubadhirifu wa rasilimali za umma.
Kiongozi wa Nchi alibainisha kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya, wakulima waliweza kupokea mbolea yao kutoka kwa Serikali bila kuingiliwa na makampuni ambayo yalinunua kwa bei nafuu na kuwauzia kwa bei ya juu.
“Mpango wa mwaka huu wa ruzuku ya mbolea ndio uliofaulu zaidi kwani wakulima walitumia vocha za mtandaoni kupata bidhaa hiyo. Hii ndiyo sababu madalali na makampuni ya biashara hawakuwa na nafasi katika zoezi hilo,” alisema Rais Ruto.
Dkt Ruto alisema ana imani kuwa mswada wa huduma ya afya kwa wote, ambao uko Bungeni, ukipitishwa na kuwa sheria utatekelezwa ipasavyo kwa sababu utatekelezwa kwa njia ya kidijitali.
Alisema Serikali imejizatiti kulinda mustakabali wa nchi kwa kutumia teknolojia ili kutoa suluhisho ambazo zinaboresha maisha na ustawi wa binadamu, kuweka uchumi wa ushindani, wa aina mbalimbali na wenye nguvu na kuimarisha ukakamavu na usalama wa jamii na taifa dhidi ya vitisho vyote.
Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, ametumia hafla nyingi kutoa hoja kali kwa wawekezaji, mashirika ya kimataifa na makampuni ya teknolojia kuhamishia mwelekeo wao wa kimkakati kwa Afrika, bara changa, la kijani kibichi la siku zijazo, kwa kufanya hivyo, kutumia faida ya kijiografia ya Kenya kama lango la kanda na bara hili.
“Mazingira ya fursa yanajitokeza katika bara letu. Soko kubwa la watu bilioni 1.4 limeibuka chini ya Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika na maeneo ya kikanda mbalimbali ya kiuchumi yanayoingiliana,” akasema Dkt Ruto.
Alisema kuwa idadi ya watu zaidi barani Afrika ni vijana, wasomi, wenye ujuzi na wenye ari.
Rais Ruto aliongeza kuwa bara la Afrika lina rasilimali nyingi za asili, ikiwa ni pamoja na madini muhimu yanayohitajika na mabadiliko ya kimataifa ya kuwa viwanda safi na vya kijani.
“Bara letu pia lina uwezo mkubwa wa nishati mbadala,” alisema.
Waziri la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Eliud Owalo alisema wizara yake itaendelea kushirikiana na sekta ya kibinafsi katika masuala ya utafiti kwa nia ya kukidhi mahitaji ya kiteknolojia ya nchi.
Balozi wa Marekani nchini Kenya Meg Whitman alisema makampuni kutoka Marekani yatatumia fursa nchini Kenya kwa manufaa ya pamoja ya raia wa nchi hizo mbili.
Aliipongeza Serikali ya Rais Ruto kwa kuweka mazingira mwafaka kwa IBM miongoni mwa makampuni mengine kuanzisha vituo vyao vya kufanya kazi nchini.
“Kenya itaendelea kuwa mahali pazuri kwa makampuni ya Marekani kutafuta fursa katika sekta mbalimbali za uchumi,” alisema Balozi Whitman.