Mkewe Rais Rachel Ruto amesema serikali inakusudia kuhakikisha kila mtoto nchini anapata elimu bora.
Rachel alitoa hakikisho hilo alipoelezea mabadiliko yanayofanywa katika sekta ya elimu na utengaji wa fedha zinazojumuisha ongezeko la hivi karibuni la msaada wa masomo kupitia mswada wa marekebisho ya hazina ya kitaifa ya ustawishaji wa maeneo bunge kutoka asilimia 35 hadi 40.
Aidha aligusia kuongezwa maradufu kwa mpango wa lishe shuleni kutoka shilingi bilioni 2 hadi bilioni 4 katika bajeti ya mwaka 2023-2024.
Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa shule ya Midas huko Eldoret Mashariki, Mkewe Rais alitoa wito wa uwekezaji zaidi katika sekta ya elimu ili kupiga jeki juhudi za serikali za kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wote nchini.
Alisema uwekezaji kama huo pia hubuni nafasi za ajira na fursa za mtungo wa usambazaji kwa jamii ya biashara ya maeneo husika.
Kupitia mpango wa Mama Doing Good, Rachel anaunga mkono idadi ya watoto wanaojiunga na shule, wanaohudhuria masomo na kuendelea na masomo hayo kupitia mpango unaojulikana kama “Mama Feeding,” huu ukiwa ni mpango wa umma wa utoaji lishe kwa watoto walio hatarini katika maeneo yasiyojiweza kiuchumi mijini na mashinani.