Edmund Serem aliongoza Kenya kutwaa nishani za dhahabu na fedha katika fainali ya mita 3,000 kuruka viunzi na maji ,huku makala ya 20 ya mashindano ya Riadha kwa chipukizi chini ya umri wa miaka 20 yakikamilika mapema Jumapili mjini Lima,Peru.
Serem, ambaye ni mshindi wa nishani ya fedha ya Afrika amenyakua dhahabu akiweka rekodi mpya ya mashindano hayo ya dakika 8 sekunde 15.28, huku mwenzake Mathew Kosgei akishinda fedha kwa dakika 8 sekunde 17 .46, wakati Hailu Ayalew wa Ethiopia akiridhika na nishani ya shaba.
Hata hivyo matumaini ya kenya kushinda medali katika fainali ya mita 1,500 yaliyeyuka baada ya Mary Nyaboke na Mirriam Chemutai wakimaliza katika nafasi za 10 na 14 mtawalia.
Saron Berhe wacEthiopia, Rachel Forysth wa Canada na Jolanda Kallabis kutoka Ujerumani walitwaa dhahabu,fedha na shaba mtawalia.
Josphat Kipkirui aliambulia nafasi ya nne katika fainali ya mita 1,500 iliyoshindwa na Mwethiopia Abdiya Fayisa, aliyeshinda dhahabu ya pili kwa kutumia dakika 3 sekunde 40.51,akifuatwa na Cameron Myers wa Australia na Alex Pintado Uhispania katika nafasi za pili na tatu mtawalia.
Kenya ilimaliza katika nafasi ya 6 kwa medali 7 dhahabu 3 fedha 3 na sahab 1.
Washindi wa dhahabu za Kenya walikuwa Sarah Moraa katika mita 800,Andrew Kiptoo Alamisi katika mita 5,000 na Edmund Serem katika mita 3,000 kuruka viunzi na maji.
Walioishindia Kenya medali za fedha ni pamoja na Mathew Kosgei katika mita 3,000 kuruka viunzi na maji ,Denis Kipkoech na Marion Jepng’etich katika mita 3,000, huku Diana Chepkemoi akitwaa shaba pekee katika mita 3,000 kuruka viunzi na maji.
Marekani ilinyakua ubingwa wa jumla kwa medali 16,dhahabu 8,fedha 4 na shaba 4.
Ethiopia ilimaliza ya pili kwa dhahabu 6 fedha 2 na shaba 2, wakati China ikihitimisha tatu bora kwa dhahabu 4 ,fedha 4 na shaba 3.
Makala ya 21 ya mashindano hayo yataandaliwa mwaka 2026 nchini Marekani.