Seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago, amekamatwa na maafisa wa polisi saa chache baada ya mahakama kutoa kibali cha kukamatwa kwake, kuhusiana na sakata ya ufadhili wa masomo ya wanafunzi waliotarajiwa kuenda nchini Finland na Canada.
Mandago alitiwa nguvuni mjini Eldoret na kusafirishwa hadi Nakuru ili kuhojiwa na maafisa wa polisi.
Seneta huyo hapo awali alifutilia mbali habari kwamba kibali cha kumkamata kimetolewa na maafisa wa polisi, akisema kuwa hakuwa mafichoni.
Mandago anatuhumiwa kwa kufuja mamilioni ya pesa ya wanafunzi waliotarajiwa kuenda kusomea katika nchi za Canada na Finland alipohudumu kama Gavana wa kaunti hiyo.
Wanafunzi hao pamoja na wazazi wao wamekuwa wakifanya maandamano mjini Eldoret na kwingineko kushinikiza kuwajibishwa kwa waliofuja pesa zao.
Mahakama ilikuwa imetoa kibali cha kukamatwa kwa Seneta Jackson Mandago na watu wengine watatu kuhusiana na sakata hiyo.
Watatu hao ni Joseph Kipkemoi Maritim, Meshak Rono na Joshua Kipkemoi Lelei.
Wanatarajiwa kukabiliwa na mashtaka ya kughushi, kutumia vibaya mamlaka na kufanya njama ya kuiba.
Washukiwa wanatuhumiwa kwa kufanya njama ya kuiba shilingi bilioni 1 kutoka kwenye akaunti iliyopo kwenye benki ya KCB iliyosajiliwa chini ya Hazina ya Uasin Gishu.