Home Kimataifa Save the Children: Watoto waliopoteza makazi Kenya 2022 waliongezeka mara saba

Save the Children: Watoto waliopoteza makazi Kenya 2022 waliongezeka mara saba

0
Mkurugenzi wa shirika la Save the Children nchini Kenya na Madagascar, Yvonne Arunga akitoa wasilisho
Mkurugenzi wa shirika la Save the Children nchini Kenya na Madagascar, Yvonne Arunga akitoa wasilisho
kra

Idadi ya watoto nchini Kenya waliopoteza makazi  kutokana na majanga yaliyosababishwa na tabia nchi iliongezeka mara saba mwaka jana.

Shirika la Save the Children limesema hayo wakati watunga sera wakikutana jijini Nairobi kujadili suluhu kwa janga la tabia nchi wakati wa Kongamano la siku tatu la Afrika kuhusu Tabia Nchi.

kra

Kwa kuzingatia tathmini ya Kituo cha Ndani cha Ufuatiliaji wa Waliopoteza Makazi, IDMC, watoto wasiopungua 187,000 walipoteza makazi nchini Kenya kutokana na majanga yaliyosababishwa na tabia nchi mwishoni mwa mwaka 2022.

Hii kwa kulinganisha na watoto 27,000 waliopoteza makazi kutokana na majanga sawia mnamo mwaka wa 2021.

Baadhi ya watoto hao walipoteza makazi mara nyingi wakati wengine wakipoteza mara moja tu.

Lakini wote hawakuwa na mahali pa kuishi kufikia mwishoni mwa mwaka jana na kulazimika kuishi kwenye kambi na makazi mengine ya muda.

Tathmini hiyo inaashiria kuwa idadi hiyo inaweza kuwa juu zaidi, kwani idadi ya watoto hao ni ya kutoka kaunti nne za Garissa, Isiolo, Marsabit na Turkana.

“Athari ya majanga yaliyosababishwa na tabia nchi kwa watoto inatia hofu. Wakati watoto wanapoteza makazi yao, wanapoteza karibu kila kitu: wanashindwa kupata huduma za afya, elimu, chakula na usalama. Pia wanapoteza viungo muhimu vinavyohitajika kwa uthabiti wao wa akili na hisia na kuwa na afya nzuri, kama vile hisia ya hali ya kawaida, marafiki na haki ya kucheza,” alisema Yvonne Arunga, ambaye ni Mkurugenzi wa shirika la Save the Children nchini Kenya na Madagascar.

Kikanda, idadi ya visa vipya vya watu kupoteza makazi ndani ya nchi kote katika eneo la Sahara barani Afrika mnamo mwaka 2022 kutokana na majanga kama hayo ilikuwa mara tatu zaidi kuliko mwaka uliotangulia, huku watu milioni 7.4 wakipoteza makazi mwaka 2022 ikilinganishwa na milioni 2.6 mwaka 2021.

Website | + posts