Home Burudani Sarah Hassan afurahia baada ya kuangaziwa na jarida la Forbes Africa

Sarah Hassan afurahia baada ya kuangaziwa na jarida la Forbes Africa

0
kra

Mwigizaji wa Kenya Sarah Hassan amejawa na furaha baada ya kuangaziwa na jarida la Forbes Africa. Jarida hilo huchukuliwa kuwa la hadhi ya juu.

Huwa linaangazia watu wa bara Africa waliobobea kwenye nyanja mbali mbali kama vile biashara, uwekezaji, teknolojia, ujasiriamali, uongozi na hata mitindo ya maisha.

kra

Makala kumhusu yalikuwa yamepatiwa mada, ” Mwigizaji na mwandalizi wa filamu wa Kenya kuhusu kuwa na majukumu mengi na ni kwa nini muda ni kila kitu”.

Hassan ambaye ameigiza kwenye vipindi kadhaa na filamu nchini Kenya na nje alichapisha video iliyoonyesha jarida hilo likifunguliwa na kuonyesha makala kumhusu.

Alishukuru sana jarida hilo kwa kumwangazia huku akielekeza wafuasi wake kwenye tovuti yake ambayo ina wasifu wake.

Kulingana na jarida la Forbes, Sarah Hassan ambaye alianza na uigizaji kabla ya kuingilia utangazaji na uaandaaji wa filamu huwa hajiwekei vikwazo kuhusu kile ambacho anaweza kuafikia.

“Baada ya kugundua kwamba anapenda kuigiza akiwa na umri mdogo, Sarah alijiunga na kundi la uigizaji lililohusika kwenye kipindi Tahidi High, ambapo aliigiza kama Tanya. Igizo hilo lilimshindisha tuzo ya mwigizaji bora wa kike kwenye tuzo za CHAT mwaka 2010 na 2011.” ndiyo baadhi ya maneno kwenye makala hayo yaliyoandikwa na Nicole Pillay.

Sarah alianza kuigiza akiwa na umri wa miaka mitano tu.

Kazi alizofanya baada ya Tahidi High zilimshindia tuzo kadhaa ikiwemo ile ya mwigizaji bora wa kike katika jukumu kuu mwaka 2014, tuzo ya mtangazaji bora wa kipindi cha runinga katika tuzo za Kalasha mwaka 2014,mwanahabari bora wa Afrika Mashariki mwaka 2015 kati ya nyingine nyingi.

Mwaka 2016 alienda Marekani ambako alikaa kwa muda wa miaka miwili unusu akinoa makali yake katika tasnia ya filamu kwa njia ya masomo.

Sasa anamiliki kampuni yake ya kuandaa filamu kwa jina Alfajiri ambayo imeandaa filamu kama “The Company you keep”, “Plan B”, “Reflections”, “Just In Time” na “Anyango And The Ogre”.

Baadhi ya kazi zake zinaonyeshwa kwenye jukwaa la Netflix.

Website | + posts