Home Habari Kuu Sanamu ya Mwalimu Nyerere yazinduliwa

Sanamu ya Mwalimu Nyerere yazinduliwa

0

Umoja wa Afrika AU hivi leo umezindua sanamu ya Rais wa kwanza wa taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika makao makuu ya umoja huo jijini Addis Ababa, nchini Ethiopia.

Hafla hii inajiri wakati viongozi wa mataifa ya Afrika wanaendeleza mkutano wao wa 37 na dhamira yake ni kutoa heshima kwa hayati Nyerere kwa juhudi zake katika ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.

Mwalimu Nyerere anafahamika pia kwa kupigania amani na usalama katika bara zima la Afrika na rais wa sasa wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliongoza uzinduzi wa sanamu yake.

Katika makao makuu ya Umoja wa Afrika kuna jengo la amani na usalama lililopatiwa jina la Julius Nyerere na lilizinduliwa Oktoba 12, 2016.

Pendekezo la kuwa na sanamu ya Nyerere nje ya jengo hilo lilitoka kwa hayati Robert Mugabe, rais wa zamani wa Zimbabwe kwenye mkutano wa 35 wa viongozi wa nchi za Afrika Agosti 2015 jijini Harare, nchini Zimbabwe.

Nyerere aliaga dunia Oktoba 14, 1999 akiwa na umri wa miaka 77. Aliongoza nchi jirani ya Tanzania kati ya mwaka 1961 na mwaka 1985.

Alianza kama waziri mkuu wa Tanganyika kisha akawa Rais na akaendelea kuwa Rais ilipobadili jina na kuwa Tanzania.

Mugabe alianzisha mchakato wa kuenzi viongozi wa nchi wanachama wa shirika la maendeleo katika eneo la Afrika Kusini SADC kwa juhudi zao katika ukombozi wa eneo hilo na bara zima.

Sanamu ya Kwame Nkrumah wa Ghana ilizinduliwa mwaka 2019 na ile ya Haile Selassie wa Ethiopia ikazinduliwa mwaka 2012.