Samson Opiyo aliishindia Kenya nishani ya kwanza kwenye michezo ya Olimpiki ya walemavu mjini Paris, baada ya kunyakua nishani ya fedha katika shindano la kuruka kwa kuchupa la T37.
Opiyo aliruka umbali wa mita 6.20 katika uwanja wa Stade de France na kuyakua nishani ya fedha na pia kuandikisha rekodi ya Bara Afrika.
Alimaliza wa pili nyuma ya Brian Lionel wa Argentina na Mbrazil Cardoso Mateus aliyenyakua nishani ya shaba.
Hii ilikuwa ni nishani ya kwanza ya Kenya ya mashindano ya viwanjani tangu mashindano ya Olimpiki ya walemavu ya Beijing mwaka 2008 wakati Mary Nakhumicha alinyakua nishani ya fedha katika urushaji sagai.
Opiyo mwenye umri wa miaka 28, alianza kushiriki mashindano ya riadha ya walemavu mwaka 2017 na kunyakua nishani ya fedha katika kitengo cha T37 mita 200 na nishani ya shaba katika kitengo cha T37 mita 100 kwenye mashindano ya kimataifa ya riadha mwaka 2019 mjini Marrakesh Morocco.