Home Michezo Safaricom yazindua awamu ya 4 ya mashindano ya chapa dimba eneo la...

Safaricom yazindua awamu ya 4 ya mashindano ya chapa dimba eneo la mashariki

Vijana wamehimizwa wajihusishe na michezo badala ya kuangazia tu masomo ya vitabu kwa sababu michezo inalipa vizuri siku hizi.

Akizungumza huko Meru kwenye hafla ya kuzindua fainali za awamu ya 4 ya mashindano ya soka ya Chapa Dimba katika eneo la mashariki mwa nchi, meneja wa kampuni ya mawasiliano nchini Safaricom katika eneo la Mlima Kenya James Mutisya aliwasihi vijana kutumia mashindano kama hayo kuboresha talanta zao ili ziwe ajira.

Mutisya alielezea kwamba fainali za mashindano ya Safaricom Chapa Dimba tayari zimeandaliwa katika maeneo ya Rift Valley na Nyanza na za eneo la mashariki zitaandaliwa Disemba 9 na 10, 2023 katika uwanja wa Kinoru mjini Meru.

Eneo la mashariki lina kaunti 8 ambazo ni Meru, Tharaka Nithi, Embu, Isiolo, Machakos, Kitui, Marsabit na Makueni.

Kando na Chapa Dimba, Mutisya alisema kwamba Safaricom imekuwa ikiandaa mipango ya matibabu bila malipo kwa ushirikiano na serikali za kaunti.

Wikendi iliyopita, wagonjwa zaidi ya 3000 walihudumiwa katika shule ya msingi ya Mitunguu katika eneo la Imenti Kusini kaunti ya Meru.

Wiki hii kampuni hiyo inaandaa mafunzo kwa waendeshaji bodaboda huko Embu kuhusu namna ya kusimamia mapato yao.

Katika miaka ya awali, washindi wa Chapa Dimba walikuwa wanapata zawadi za thamani ya milioni 10 lakini kulingana na Mutisya pesa hizo zimeongezwa hadi milioni 20.

Mchezaji wa timu ya KCA FC ya Meru Elijah Mwanza, alishukuru Safaricom kwa mashindano hayo ambayo yanalenga kukuza talanta za soka huku akihimiza kampuni nyingine kuiga mfano huo.

Website | + posts
Jeff Mwangi
+ posts