Home Biashara Safari za ndege za uchukuzi wa mizigo zarejelea katika uwanja wa Eldoret

Safari za ndege za uchukuzi wa mizigo zarejelea katika uwanja wa Eldoret

Safari za ndege za uchukuzi wa shehena hadi kwenye uwanja wa ndege wa Eldoret, zimerejelewa huku mawaziri wawili wakitoa hakikisho kwamba serikali inaratibu mikakati ya kuimarisha uwanja huo wa ndege kufikia viwango vya kimataifa.

Waziri wa barabara na uchukuzi Kipchumba Murkomen na mwenzake wa uwekezaji na viwanda Moses Kuria, walizindua tena safari hizo huku ndege ya shirika la Ethiopia ya uchukuzi wa shehena ikiwa ya kwanza kutua.

Shughuli za uchukuzi wa shehena kwenye uwanja huo zilikuwa zimesitishwa kwa muda wa miezi mitatu iliyopita.

Mawaziri hao wawili walitoa hakikisho kwamba serikali itasuluhisha haraka baadhi ya changamoto zilizoko ili kuhakikisha shughuli za usafirishaji shehena kwenye uwanja huo hazitatiziki tena.

Kwenye mkutano na chama cha wachukuzi shehena wa kimataifa humu nchini, Murkomen alisema kuwa serikali inatekeleza mipango ya kuimarisha uwanja huo wa ndege na kwamba wizara yake inashirikiana kwa karibu na halmashauri ya viwanja vya ndege nchini, KAA, na tume ya taifa ya ardhi ili kuimarisha uwanja huo.