Home Kimataifa Rwanda: Kifo cha Anne Rwigara – “Ni fumbo” – mama yake Adeline

Rwanda: Kifo cha Anne Rwigara – “Ni fumbo” – mama yake Adeline

0
Anne Uwamahoro Rwigara akipelekwa na polisi katika mahakama ya Kigali tarehe 10, Oktoba 2017

Anne Rwigara, mmoja wa watoto wa mfanyabiashara maarufu wa zamani nchini Rwanda, Assinapol Rwigara, amefariki nchini Marekani alikokuwa akiishi, kwa mujibu wa wanafamilia wake.

Mwanafamilia wa karibu aliambia BBC Idhaa ya Maziwa Makuu kwamba Anne alikufa muda mfupi baada ya kujifungua nyumbani kwake huko California.

Mamake Adeline Rwigara, anayeishi Kigali, aliambia BBC kwa maandishi: “Hakuwa mgonjwa. Kifo chake ni fumbo.”

Anne Uwamahoro Rwigara, ambaye alikuwa na umri wa miaka 41 – kulingana na wasifu wake alioutoa mahakamani mnamo 2017 – anakumbukwa mwaka huo alizuiliwa gerezani kwa siku kadhaa pamoja na mama yake Adeline na dadake mkubwa Diane Rwigara wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali.

Ilikuwa baada ya uchaguzi wa urais wa 2017 ambapo dadake mkubwa Diane alizuiwa kuwania nafasi hiyo.

Rais Paul Kagame alishinda uchaguzi huo kwa karibu 99% ya kura.

Hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu chanzo cha kifo cha Anne Rwigara, ambaye alikuwa raia wa Marekani kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.

Baba yake Assinapol Rwigara alikuwa mmoja wa wafanyabiashara maarufu nchini Rwanda kwa karibu miaka 40 hadi kifo chake mnamo 2015.

Kifo chake kilikumbwa na utata, polisi wa Rwanda walisema alifariki katika ajali ya barabarani.

Familia yake ambayo inadai kuwa aliuawa katika ajali iliyopangwa, ilimwandikia barua Rais Kagame ikimtaka achunguze kifo cha Assinapol, ikisema kuwa kuna jambo ambalo haikubaliani na chama tawala.

BBC
+ posts