Serikali itarejelea ujenzi wa barabara za Mau Mau zenye urefu wa kilomita 200.
Rais William Ruto amesema serikali imezipiga dafrau changamoto za madeni ambazo zilikuwa zimechelewesha mipango mikuu ya maendeleo, zikiwemo barabara za Mau Mau.
Alisema barabara hizo zitarahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa, kuwezesha biashara na kuchochea ukuaji uchumi.
Kiongozi wa nchi aliyasema hayo katika eneo la Nyambari, eneo bunge la Lari katika kaunti ya Kiambu wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Uplands-Kijabe-Maai Mahiu.
Rais pia aliweka jiwe la msingi katika soko la Soko Mjinga katika eneo bunge hilo.
Soko hilo litawapa mazingira bora wafanyabiashara na walaji ambao wamekuwa wakiendeshea shughuli zao kwenye barabara kuu yenye shughuli nyingi ya Nairobi-Naivasha.
Baadaye, Rais Ruto alizindua Chuo cha Mafunzo ya Utabibu cha Kenya huko Kangema katika kaunti ya Murang’a.
Alisisitiza nia ya serikali kuhakikisha Wakenya wanapta huduma bora za matibabu.
Naibu Rais Rigathi Gachagua, Gavana wa kaunti ya Kiambu Kimani Wamatangi na wabunge wakiongozwa na kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wah ni miongoni mwa viongozi waliokuwapo.