Home Habari Kuu Ruto: Tumejitolea kulinda maslahi ya wafanyakazi

Ruto: Tumejitolea kulinda maslahi ya wafanyakazi

0

Kiongozi wa nchi Rais William Ruto amesema kwamba serikali imejitolea kulinda maslahi ya wafanyakazi nchini ili kuafikia viwango vilivyowekwa kimataifa.

Alikuwa akizungumza kwenye awamu ya tano ya kongamano la shirikisho la kimataifa la vyama vya wafanyakazi barani Afrika jijini Nairobi.

Kulingana naye, serikali inatambua mahusiano mema na wafanyakazi na ulinzi wa jamii kama haki za kibinadamu na uhuru wa kimsingi.

Alisema hilo linadhihirika kupitia namna yao ya uongozi ambayo mizizi yake iko katika mpango wa kuwezesha watu wa chini kiuchumi almaarufu “Bottom-Up Economic Transformation Agenda”.

Mpango huo alisema unatambua kwamba uwezeshaji wa watendakazi ndio nguzo kuu katika uimarishaji wa nchi hii kiuchumi.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na waziri wa Leba Florence Bore, mkurugenzi mkuu wa shirikisho la kimataifa la vyama vya wafanyakazi Gilbert Houngbo, Katibu mkuu wa shirikisho hilo Kwasi Adu-Amankwah, Rais wa shirikisho hilo Mody Guiro, Martha Molema na katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli kati ya wengine wengi.

Awali viongozi wa shirikisho hilo la vyama vya wafanyakazi walimzuru Rais Ruto katika ikulu ya Nairobi.

Rais alisifia shirikisho hilo kwa kutekeleza jukumu muhimu la kuhakikisha haki kwa wafanyakazi barani Afrika.

Bwana Gilbert Houngbo alisifia mpango wa serikali wa huduma bora za afua kwa wote na mipango ya kuingia kwenye mikataba ya utendakazi na nchi nyingine.

Website | + posts