Home Habari Kuu Ruto: Serikali kuwekeza vilivyo kwa ujenzi wa taifa

Ruto: Serikali kuwekeza vilivyo kwa ujenzi wa taifa

0
Serikali ina nia ya kuwezesha Wakenya kushiriki ipasavyo katika ujenzi wa nchi.
Rais William Ruto amesema kupatikana kwa fursa zilizokusudiwa kutaleta utajiri na kuboresha maisha ya watu.
Alisema hayo leo Jumatatu katika Benki Kuu ya Kenya (CBK), Nairobi, wakati wa uzinduzi wa Hifadhi Kuu ya Dhamana (DhowCSD).
 Muundombinu huo unaruhusu wafanyabiashara katika dhamana za serikali katika masoko ya fedha ya ndani, kikanda na kimataifa kufanya miamala ya kielektroniki.
 Ukimilikiwa na CBK, mfumo huu unawezesha uhifadhi wa pamoja wa dhamana na usasishaji salama wa hali ya miamala inayohusiana nazo.
 “Uendelezaji wa DhowCSD unaimarisha mpango wa serikali wa kuondoa vizuizi vya biashara,” alisema Rais Ruto.
 Alisema kuwa jukwaa hilo litakuza soko la mitaji la ndani, na kukuza akiba na uwekezaji.
 “Pia itakuza ukuaji na utulivu wa soko letu la kifedha,” aliongeza Rais.
 Aliandamana na Mawaziri Njuguna Ndung’u wa Fedha na Moses Kuria wa Biashara na Gavana wa CBK Kamau Thugge.
 Rais Ruto alibainisha kuwa mfumo huo mpya utaleta urahisi, ufanisi na kasi bila kuathiri usalama.
 Alieleza kuwa wawekezaji hawatalazimika tena kujiwasilisha wenyewe katika CBK ili kupitia mchakato wa kufungua akaunti ya CDS.
 Tovuti ya mwekezaji wa CSD na programu ya simu imefungua ufikiaji wa soko la dhamana kwa kila mtu, bila kujali tabaka.
 Kama vile Hazina ya Hasla, huduma za kiotomatiki kupitia mifumo ya kidijitali imefungamanishwa na dhamira ya serikali ya kupanua fursa kwa Wakenya.
 “Tunaamini hii itaendesha uchumi wetu kutoka chini kwenda juu.”
 Prof. Ndung’u alisema kuzinduliwa kwa DhowCSD ni hatua muhimu ambayo itaboresha soko.
 Kwa upande wake, Gavana wa CBK alidokeza kuwa mfumo huo utaongeza ufanisi wa kazi katika soko la ndani na kuongeza usambazaji wa ukwasi.
PCS
+ posts