Home Habari Kuu Ruto: Serikali inashughulikia suala la gharama ya maisha

Ruto: Serikali inashughulikia suala la gharama ya maisha

0

Rais William Ruto anasema utawala wake unachukua hatua za makusudi zinazonuia kukabiliana na gharama ya juu ya maisha wanayokumbana nayo Wakenya. 

Amekiri kuwa familia nyingi zimeelemewa na gharama ya juu ya maisha.

“Gharama ya juu ya maisha si suala la dhahania. Ni ukweli zinaokumbana nazo familia nyingi, na ambalo linaweza kuangaziwa kupitia hatua za kivitendo na madhubuti,” alisema Rais Ruto wakati akiwahutubia Wakennya kupitia kikao cha pamoja cha bunge leo Alhamisi.

“Moja ya hatua bora zaidi za kukabiliana na gharama ya juu ya maisha ni mkakati wa kuunga mkono kilimo ili kuhakikisha uzalishaji wa chakula.”

Alisema kupitia hatua zilizochukuliwa na utawala wake kama vile utoaji wa mbolea ya bei nafuu, uzalishaji wa mahindi umeongezeka nchini kwa ziada ya magunia milioni 18.

Hatua hiyo, alisema, imesababisha kupungua kwa bei ya pakiti moja ya kilo mbili ya unga wa mahindi kutoka shilingi 250 hadi kati ya shilingi 145 na 175.

Kiongozi wa nchi aliongeza kuwa ili kuhakikisha uwazi na umakinifu katika usambazaji wa mbolea ya bei nafuu kwa wakulima, kuna haja ya kuanzisha sajili ya kidigitali ya wakulima.