Rais William Ruto amesema kwamba mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na Umoja wa Ulaya, EU ni kilele cha ushirikiano ambao umekuwepo wa aina hiyo kati ya Kenya na nchi 27 wanachama wa umoja huo.
Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi baada ya mkataba huo kutiwa saini, Rais Ruto aliahidi kwamba Kenya itahakikisha kwamba bidhaa ambazo itauza kwa nchi za EU ni za ubora wa kiwango cha juu.
Kiongozi wa nchi alitaja kujitolea kwa Kenya na mataifa ya EU kwa uhuru wa kuchagua, kuheshimu sheria, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuheshimu haki za kibinadamu kumeboresha hata zaidi ushirikiano na nchi hizo.
Kwa mara nyingine, alitaja nia ya serikali ya kuhakikisha wahusika wa bidhaa zinazouzwa nje wanapata mapato bora wakiwemo wakulima na hata wanaounda bidhaa za chuma na mbao.
Rais Ruto alikaribisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC kujiunga na Kenya ili kufaidi kutokana na mkataba huo wa ushirikiano wa kiuchumi na Umoja wa Ulaya, matamshi yaliyokaririwa na Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen.
Von der Leyen alisema mkataba huo ni wa kuimarisha hata zaidi uhusiano wa kiuchumi ambao umekuwepo kati ya EU na Kenya akisema mwaka jana pekee, biashara kati ya EU na Kenya ilikuwa ya thamani ya Euro bilioni 3.
Mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya EU na Kenya uliafikiwa baada ya mashauriano ambayo yalikamilika Juni 19, 2023.
Unalenga kuimarisha biashara ya bidhaa na kubuni fursa mpya za kiuchumi, ushirikiano unaolenga kupiga jeki ukuaji wa kiuchumi wa taifa la Kenya.
Baadhi ya mambo yaliyo kwenye mkataba huo ni kufunguliwa kwa masoko ya EU kwa bidhaa za Kenya, kumotisha uwekezaji wa EU nchini Kenya, kusimamia biashara thabiti na endelevu, kuweka masharti thabiti kuhusu masuala ya leba, usawa wa kijinsia, utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.