Home Habari Kuu Ruto: Mfumo mpya wa fedha utasaidia dunia kushinda umaskini na mabadiliko ya...

Ruto: Mfumo mpya wa fedha utasaidia dunia kushinda umaskini na mabadiliko ya tabia nchi

0

Rais William Ruto amesema mfumo wa fedha unapaswa kuwa wenye usawa.

Ameelezea kuwa rasilimali hazipaswi kudhibitiwa na Benki ya Dunia wala Shirika la Fedha Duniani, IMF.

“Afrika haitaki chochote bila malipo. Lakini tunahitaji mfumo wa fedha usioweka madaraka mikononi mwa watu wachache.”

Alisema hatua hiyo itahakikisha kuwa “sisi sote tunapata rasilimali kwa usawa”.

Ruto alisema dunia haiwezi ikaendelea kama kawaida wakati mambo hayasongi mbele.

Aliyasema hayo leo Alhamisi wakati wa kikao na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Mkurugenzi Mkuu wa IMF Kristalina Georgieva na Rais wa Kundi la Benki ya Dunia Ajay Banga wakati wa Mkutano wa Makubaliano Mapya ya Fedha Duniani unaofanyika mjini Paris nchini Ufaransa.

Akirejelea wito wa Rais Ruto juu ya haja ya kuufanyia mapitio mfumo wa fedha duniani, Rais Macron alisema mtazamo wenye ujasiri na mpana unaweza ukaibadili dunia.

Alisema wakati pia umewadia wa kuzingatia uwezo endelevu wa nchi kulipa madeni na athari za mabadliko ya tabia nchi.

“Tunahitaji njia mbalimbai lakini jumuishi kuhusiana na mabadiliko ya tabia nchi ili kutatua suala hilo. Hakuna anayepaswa kuachwa nyuma; sio hata China,” alielezea Rais Macron.

Alitoa wito wa Benki ya Dunia na IMF kufanyiwa mabadiliko kuhusiana na namna zinazyoendesha shughuli zao hususan kwa kuzingatia uhalisia wa mambo.

“Hii inapaswa kufanywa haraka na kwa dharura.”

Viongozi wa nchi wapatao 50 sambamba na taasisi za kimataifa na wawakilishi wa mashirika ya kijamii wanahudhuria mkutano huo.

Unadhamiria kubuni mfumo mpya wa fedha duniani ili nchi zinazoathiriwa ziwezeshwe ipasavyo kukabiliana na umaskini na mabadiliko ya tabia nchi.

Awali, Rais Ruto alifanya mkutano na Rais wa Colombia Gustavo Petro ambapo walikubaliana kutafuta nyanja mpya za ushirikiano kama vile biashara na kilimo.

Pia alijadili mpango wa Kenya wa kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO Tedros Adhanom.

Baadaye, alikutana na Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry ambapo masuala ya maslahi ya pande mbili yalijadiliwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here