Home Habari Kuu Ruto kuongoza taifa katika zoezi la upanzi wa miti

Ruto kuongoza taifa katika zoezi la upanzi wa miti

0

Rais William Ruto leo Jumatatu atazindua zoezi la upanzi wa miti kote nchini katika eneo la Makindu, kaunti ya Makueni. 

Serikali imetangaza Novemba 13 kuwa sikukuu ya upanzi wa miti.

Inalenga kupanda angalau miti milioni milioni 500 siku hiyo na miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032.

Kila Waziri ataongoza shughuli za upanzi wa miti katika kaunti mbili.

Waziri wa Mazingira Soipan Tuya ataongoza shughuli ya upanzi miti katika kaunti ya Vihiga wakati mwenzake wa Habari na Mawasiliano Eliud Owalo akiongoza shughuli hiyo katika kaunti za Nandi na Kisii.

Waziri wa Madini Salim Mvurya atakuwa katika kaunti za Tana River na Lamu kuongoza shughuli hiyo wakati Waziri wa Uchukuzi na Barabara Kipchumba Murkomen akikita kambi katika kaunti za Homa Bay na Mombasa.

Na huku mawaziri wakitua kaunti mbalimbali kuhakikisha azima ya serikali ya kupanda miti bilioni 15 katika kipindi cha miaka 10 ijayo inatimia, Katibu katika Wizara ya Usalama wa Kitaifa Dkt. Raymond Omollo anatoa wito kwa Wakenya kote nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo la upanzi wa miti.

“Wakenya wanaombwa kufika ofisi ya Chifu iliyo karibu nao kuchukua miche watakayopanda,” amesema Dkt. Omollo.

Magavana, Makatibu, Makamishna wa Kaunti na maafisa wengine waandamizi serikalini ni miongoni mwa watu watakaoshiriki zoezi la upanzi wa miti leo Jumatatu.

“Makamishna wa kaunti tayari wameunda timu za mipango za kiufundi katika kaunti zao husika zikiwajumuisha wawakilishi kutoka Huduma ya Misitu ya Kenya, KFS na Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira, NEMA miongoni mwa washikadau wengine wa serikali na wasiokuwa wa serikali,” anasema Dkt. Omollo.

 

Website | + posts