Home Habari Kuu Ruto kuhutubia kikao cha pamoja cha bunge leo Alhamisi

Ruto kuhutubia kikao cha pamoja cha bunge leo Alhamisi

0

Rais William Ruto leo Alhamisi mchana atalihutubia taifa kupitia kikao cha pamoja cha bunge la Taifa la lile la Seneti. 

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Rais Ruto kulihutubia taifa kupitia kikao hicho baada ya kuibuka mshindi wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Kikao hicho kitapeperushwa mubashara na runinga ya KBC Channel 1 na idhaa mbalimbali za redio zinazomilikiwa na shirika la utangazaji nchini, KBC.

Usikose pia kutembelea tovuti za www.kbc.co.ke na www.radiotaifa.kbc.co.ke kwa taarifa za kina kuhusiana na yatakayosemwa wakati wa kikao hicho.

Kifungu 132 (1)(b) na (c) cha katiba kinamhitaji Rais kuhutubia kikao maalum cha bunge mara moja kwa mwaka.

“Wabunge wote na umma kwa jumla wanataarifiwa kuwa kikao cha pamoja cha bunge kitafanyika katika chemba ya bunge la Kitaifa katika majengo makuu ya bunge, Nairobi, Alhamisi, Novemba 9, 2023 saa nane na nusu mchana,” ilisema taarifa kutoka kwa Maspika Moses Wetang’ula wa bunge la Taifa na Amason Kingi wa bunge la Seneti Jumatatu wiki hii.

Wakati wa kikao hicho, Rais Ruto anatarajiwa kuangazia hatua zinazochukuliwa na utawala wake kuangazia changamoto mbalimbali zinazolikumba taifa ikiwa ni pamoja na gharama ya juu ya maisha.

Hususan, kupanda mara kwa mara kwa bei ya mafuta nchini kumekuwa mwiba kwa Wakenya wengi na kumekumbana na shutuma si haba.

Serikali imekuwa mstari wa mbele kuwagawia wakulima bei ya mbolea ya bei nafuu na mbegu katika hatua inayolenga kuimarisha uzalishaji wa chakula nchini.

Ingawa wakulima wameonekana kupata mavuno mengi mwaka huu kutokana na juhudi hizo, kumekuwa na lalama kuhusiana na bei ya chini ya ununuzi wa mazao hayo hususan mahindi kutoka kwa serikali.

Lalama zingine zinahusiana na matozo yanayotozwa huduma mbalimbali, ya hivi punde yakilenga sekta ya ardhi.

Aidha miradi ya miundombinu inayotekelezwa na serikali ya Kenya Kwanza chini ya mpango wake wa mabadiliko ya kiuchumi kuanzia chini hadi juu, BETA inatarajiwa kuangaziwa katika hotuba ya Rais.