Home Habari Kuu Ruto: Kilimo ni muhimu mno kwa ustawi wa nchi

Ruto: Kilimo ni muhimu mno kwa ustawi wa nchi

0

Serikali inatekeleza mabadiliko katika sekta za kilimo na mifugo kwa lengo la kufikia mabadiliko ya kiuchumi nchini.

Rais William Ruto amesema mabadiliko hayo yatawezekana tu kupitia uongezaji wa matumizi ya pembejeo na uuzaji wa ngozi kote duniani.

Rais Ruto alisema kuna haja kwa wakulima kukumbatia mchakato wa uoongezaji thamani ili kuongeza ushindani wao na mapato.

Alizungumza hayo wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya kimataifa ya kilimo ya Nairobi katika uwanja wa Jamhuri leo Jumatano.

Rais Ruto alisema serikali imeongeza matumizi ya mbegu bora na mbolea kama sehemu ya mageuzi yanayolenga kuongeza uzalishaji wa chakula na kupunguza gharama ya maisha.

Aliongeza kuwa sekta ya kilimo inasalia uti wa mgongo wa uchumi wa nchi hii na uendelezaji wa viwanda, hasa katika upatikanaji wa mapato na utoaji wa malighafi ya kutumiwa katika uzalishaji.

“Kwa hivyo, kufanyia mabadiliko uzalishaji wa kilimo ndio njia bora zaidi ya kustawisha uchumi wa nchi yetu,” alisema Rais Ruto.

Alitaja hatua kadhaa zilizochukuliwa na serikali kuibadilisha sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na utoaji wa mtaji wa kutosha na wa bei nafuu kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji.

“Pia tutawasaidia wakulima milioni mbili wanaokumbwa na uhaba wa chakula kuzalisha chakula cha ziada kupitia upatikanaji wa ufadhili wa bei nafuu wa pembejeo ili kuongeza uzalishaji.”

Kwa upande wake, Gavana wa Nairobi Johnstone Sakaja alisema uendelezaji wa sekta ya kilimo unasalia kuwa nguzo muhimuu katika kuangazia changamoto zinazoikumba nchi.

“Tutabuni mazingira mwafaka kwa wakulima wetu kando na kuanzisha masoko ya wao kuuza mazao yao,” alisema Gavana Sakaja.

Website | + posts