Home Habari Kuu Ruto: Ili kukua, Afrika lazima iwekeze kwa rasilimali watu

Ruto: Ili kukua, Afrika lazima iwekeze kwa rasilimali watu

0

Bara la Afrika lazima liwekeze kimkakati katika nguvukazi yake ili liweze kukua.

Rais William Ruto amesema bara hilo limejaaliwa na rasilimali watu wanaoweza kuchochea mabadiliko.

Alisema Afrika ni lazima ijiweke kwenye njia ambayo itahakikisha utumiaji ipasavyo wa rasilimali watu wenye ujuzi, walioelimika na wenye tija.

Hatua hiyo, alisema, itahakikisha ukuaji endelevu wa uchumi wa bara la Afrika.

“Ni lazima — kwa pamoja na nchi zingine na washirika — tubuni mpangokazi ambao kimakusudi utakuza na kuwekeza katika rasilimali watu ili kupata mafao zaidi.”

Alisema ameshawishika kwamba ikiwa Afrika itafuatilia mchanganyiko sahihi na unaofuatana wa sera, itashinda majanga ya kawaida na yanayochipuka.

“Lakini pia tutakuwa na fursa ya kubadilisha kuongezeka kwa idadi ya watu wetu na vijana ili wawe watu wenye tija,” alisema Rais Ruto.

Kulingana naye, hii itasaidia kuinadi Afrika kama bara changa na la kijani la siku zijazo na mwendeshaji wa mabadiliko mapya ya kiviwanda duniani.

Rais Ruto aliyasema hayo leo Jumatano katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Julius Nyerere mjini Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika juu ya Rasilimali Watu.

Chini ya kaulimbiu: “Uharakishaji wa Ukuaji Uchumi wa Afrika: Uongezaji wa Uzalishaji wa Vijana kwa Kuboresha Mafunzo na Ujuzi”, tukio hilo liliandaliwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu.

Rais Suluhu aliitaka Afrika kuongeza uwekezaji katika huduma za jamii kama vile elimu na afya ili kuboresha uzalishaji.

Alisema kuna hatari ya bara hilo kutilia mkazo mno majanga inalokumbana nalo na kutoangazia uwekezaji katika njanja muhimu kama vile nguvukazi.

“Ilhali, hii ndio mali kubwa zaidi ya Afrika, inayochapa kazi kwa kujituma, yenye vipaji anuai na yenye bidii ya mchwa.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here