Home Habari Kuu Ruto atoa wito kwa Wakenya kuwa wazalendo

Ruto atoa wito kwa Wakenya kuwa wazalendo

0

Rais William Ruto ametoa wito kwa Wakenya kuwa wazalendo na kudumisha maadili waliokuwa nayo watangulizi wa nchi. 

Amesema Wakenya wanapaswa kuendelea kuwa na mtazamo chanya bila kujali hali ilivyo kwa sasa, akiongeza kuwa changamoto zinazolikumba taifa zitatatuliwa.

Rais Ruto alielezea wasiwasi kuwa Kenya inapongezwa na watu kutoka nje, lakini baadhi ya Wakenya wanalitilia doa taifa lao wenyewe.

“Baadhi ya watu wanatilia chumvi baadhi ya mambo nchini badala ya kuonyesha upendo kwa nchi yao,” alilalama Rais.

Aliyasema hayo katika Ikulu Ndogo ya Eldoret, kaunti ya Uasin Gishu, alikokuwa mwenyeji wa maafisa na watoto kutoka makazi 52 kabla ya kuandaliwa kwa sherehe za Sikukuu ya Krismasi.

Alitoa mfano wa wakala wa usafiri wa Marekani kwa jina Lonely Planet aliyetambua Kenya kama mahali pazuri pa kutembelea mwaka 2024.

Alisema tathmini hiyo inayopaswa kuungwa mkono inaliweka jiji la Nairobi mbele ya majiji mengine maarufu kama vile Paris, Montreal, na Philadelphia, miongoni mwa mengine.

Kadhalika, kiongozi wa nchi alisema Benki ya Dunia imeiorodhesha Kenya kama taifa la 29 linalokua zaidi kiuchumi duniani.

Rais Ruto aidha alitoa wito kwa Wakenya kuyapa kipaumbele maslahi ya nchi ili kwa pamoja tuweze kuliweka taifa katika mwelekeo mzuri na kukuza uzalendo katika vizazi vijavyo.