Home Habari Kuu Ruto asema mfumo wa dijitali utasaidia kukomesha ufisadi

Ruto asema mfumo wa dijitali utasaidia kukomesha ufisadi

0
Serikali haitawakubalia watu wafisadi kuchelewesha uwekaji wa huduma za serikali kwenye mfumo wa dijitali, amesema Rais William Ruto.
Ameongeza kuwa serikali imejitolea kuhakikisha mpito kuelekea mfumo wa malipo wa dijitali unakamilishwa ili kukomesha ufisadi na wizi wa rasilimali za serikali.
Rais Ruto aliongeza kuwa kupunguzwa kwa zaidi ya mifumo 3,000 ya malipo ya paybill serikalini hadi kuwa moja imesaidia  kufuatilia rasilimali na kukomesha wizi.
Kulingana naye, sera mpya inayohitaji karo ya shule kulipwa kupitia mfumo wa  e-citizen itatokomeza ada zisizokuwa halali zinazotozwa na baadhi ya shule.
“Mfumo wa malipo ya pesa taslimu ni telezi na mara nyingi hutoa mwanya wa ufisadi. Teknolojia itatusadia kumaliza hili,” alisema Rais.
Kiongozi wa nchi aliyasema hayo leo Jumatano wakati wa mkutano na Wakenya wanaoishi nchini Japani.
Wakenya wanaoishi ughaibuni pia wanaweza wakafanya shughuli za serikali kupitia mfumo wa  e-Citizen.
Rais alitumia fursa hiyo kusema serikali yake inabuni nafasi za ajira kwa vijana waliopo ndani na nje ya nchi.
Alisema hitaji la Wakenya wenye ujuzi ughaibuni ni kubwa.
“Tuna shuhuda kutoka kwa kampuni ambazo zimetangamana na Wakenya walioajiriwa kuwa nguvukazi yetu ni bora zaidi,” alisema Rais Ruto.
Aliongeza kuwa serikali inapanga kuboresha huduma kwa Wakenya wanaoishi nje ya nchi ili kuboresha mchango wao kwa ukuaji wa uchumi wa nchi.
Website | + posts