Home Kimataifa Ruto amwomboleza Rais wa Iran Ebrahim Raisi

Ruto amwomboleza Rais wa Iran Ebrahim Raisi

0

Rais William Ruto amemwomboleza rais wa Iran Ebrahim Raisi aliyefariki katika ajali ya ndege Jumapili.

Ruto kupitia mtandao wa X siku ya Jumatatu alimtaja Raisi kuwa kiongozi jasiri na mtumishi wa umma aliyejitolea na kazi iliyotukuka katika utumishi wa umma.

“Ningependa kutoa rambirambi zangu za dhati na mshikamano na watu wa Iran katika wakati huu mgumu,” alisema Rais Ruto.

Alimtaja kama kiongozi dhabiti aliyejitolea kwa mambo ambayo aliamini na alijaribu kuinua msimamo wa Iran katika jukwaa la kimataifa.

Ruto aliongeza kuwa Kenya na Jamhuri ya Iran zina uhusiano wa kindugu na ziara ya Raisi nchini Kenya mwezi Julai 2023, ambayo ilikuwa safari ya kwanza barani Afrika, ilidhihirisha mshikamano kati ya nchi hizi mbili.

“Tunapowapa pole watu wa Iran, tunaomba rehema za Mwenyezi Mungu na faraja kwa watu wa Iran,” Ruto alisema.

Raisi alithibitishwa kuaga dunia Jumatatu asubuhi baada ya helikopta aliyokuwa ndani pamoja na Waziri wa Nchi za Kigeni Hossein Amir-Abdollahian na viongozi wengine kupatikana ikiwa imeteketea eneo la Kaskazini-Magharibi mwa Iran.

Taarifa za awali ziliripoti kuwa ndege hiyo iliyombeba Raisi na wasaidizi wake ilitua kwa ghafla kutokana hali mbaya ya hewa iliyosababishwa na kuenea kwa ukungu.