Home Habari Kuu Rais Ruto ampongeza Tshisekedi kwa kushinda uchaguzi wa urais DRC

Rais Ruto ampongeza Tshisekedi kwa kushinda uchaguzi wa urais DRC

0

Rais William Ruto amempongeza Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi ulioandaliwa nchini humo Disemba 20, 2023. 

Rais Tshisekedi alishinda kwa asilimia 73 ya kura zilizopigwa huku mshindani wake wa karibu mwanabiashara Moise Katumbi akipata asilimia 18 ya kura zote zilizopigwa.

“Pongezi za dhati kwa ndugu yangu Mheshimiwa Felix Tshisekedi, Rais wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, kwa ushindi uliostahiki. Uchaguzi huo ni hatua kubwa ya kidemokrasia katika historia ya taifa lako. Natazamia kuimarisha uhusiano kati ya Kenya na DRC kwa manufaa ya pande mbili ya nchi zetu,” alisema Rais Ruto katika ujumbe wake wa pongezi.

Kulingana na takwimu, wapiga kura waliojitokeza kupiga kura wakati wa uchaguzi huo ni asilimia 40, sawa na watu milioni 18.

Hata hivyo, uchaguzi wenyewe ulikumbwa na matatizo mengi ya kimpangilio ambapo vituo fulani viliongezewa muda wa kupiga kura kwa siku moja katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Vituo vingi vya kupigia kura havikufunguliwa kwa wakati na mitambo mingi ya kupigia kura ilikosa kufanya kazi siku ya kwanza ya kupiga kura.

Wengi walisubiri kwa muda mrefu kabla ya kupiga kura huku wengine wengi wakikosa subira na kurejea nyumbani bila kupiga kura.

Upinzani unahisi kwamba matatizo hayo yalipangwa kama njama ya kuiba kura na kumpendelea Rais Tshisekedi.

Wanajeshi wametumwa kwenye sehemu kadhaa mjini Kinshasa kuzuia ghasia huku wafuasi wa Tshisekedi wakisherehekea barabarani.

Wagombea kadhaa wa upinzani wamepinga matokeo hayo wakitaka uchaguzi urudiwe.

Wanaopinga matokeo hayo wana muda wa siku mbili kuwasilisha malalamishi yao katika mahakama ya kikatiba.

Mahakama hiyo itatumia muda wa siku 7 kutatua kesi hizo huku Tshisekedi akitarajiwa kuapishwa mwisho wa mwezi huu wa Januari mwaka 2024.

Website | + posts