Home Kimataifa Ruto aahidi kutekeleza ripoti ya maridhiano kikamilifu

Ruto aahidi kutekeleza ripoti ya maridhiano kikamilifu

0
Rais William Ruto
kra

Rais William Ruto amekariri kuwa atatekeleza kikamilifu ripoti ya kamati ya kitaifa ya maridhiano iliyowasilishwa kwake jana Jumapili.

Kamati hiyo iliongozwa na kiongozi wa wengi katika bunge la Taifa Kimani Ichung’wah na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka.

kra

Kamati hiyo iliwasilisha ripoti hiyo licha ya kuibuka kwa migawanyiko hasa katika mrengo wa upinzani ambapo baadhi ya wanachama wameshikilia msimamo wa kuipuuza endapo suala la kupunguzwa kwa gharama ya maisha litapuuzwa.

Akiwahutubia waumini alipohudhuria ibada jana Jumapili, Rais Ruto alisema atatekeleza mapendekezo ya ripoti hiyo kupitia kwa baraza la mawaziri na pia bunge la kitaifa.

Kiongozi wa muungano wa Azimio Raila Odinga amekiri kuipokea ripoti hiyo lakini anasema hataizungumzia kwa sasa hadi atakapoisoma na kujifahamisha yaliyomo.

Kiongozi wa chama cha Narc Kenya Martha Karua na yule wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa hata hivyo wameonekana kupuuzilia mbali ripoti hiyo wakidai ilikosa kuangazia masuala msingi yanayowaathiri Wakenya, hususan suala la gharama ya maisha.

Karua na Wamalwa ni wanachama wa muungano wa Azimio.

Huku ngome ya Azimio ikionekana kukumbwa na migawanyiko, hatima ya ripoti ya kamati hiyo iliyolenga kuwaunganisha Wakenya na kusitisha malumbano ya mara kwa mara kwa sasa haijulikani.