Awamu ya kwanza ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu katika eneo la Kibra, kaunti ya Nairobi inaendelea vyema.
Hayo yamesemwa na Rais William Ruto leo Jumatatu wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa zaidi ya nyumba 4,054 za bei nafuu katika eneo la Soweto, Kibra.
Ruto amesema amefurahishwa na kazi inayoendelea ya ujenzi.
Awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba 15,000 itaanza kabla ya mwisho wa mwaka huu huku ile ya tatu itakayohusisha ujenzi wa nyumba 20,000 ikitarajiwa kuanza mwezi Januari mwakani.
Akiwahutubia wakazi wa eneo hilo wakati wa ukaguzi huo, Rais Ruto amesema ujenzi wa nyumba za bei nafuu utaleta mabadiliko humu nchini.
Kulingana naye, ujenzi wa nyumba hizo ndio njia kuelekea maisha bora kwa Wakenya wote.
Amesema mpango huo utazipatia makumi ya maelfu ya familia fursa ya kumiliki nyumba na kubuni nafasi za ajira kwa vijana.
“Ni kupitia nyumba za bei nafuu ambapo tunaweza tukaibadilisha Kenya,” amesema kiongozi wa nchi.
Ameongeza kuwa ukamilishaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo itawawezesha wakazi wa Kibra kufikia ndoto zao za kumiliki nyumba nadhifu katika mazingira safi.
Kitaifa, Ruto amesema zaidi ya nyumba 110,00 zinaendelea kujengwa kote nchini.