Home Kimataifa Ruto: Afrika ifanye kazi kwa umoja kukabiliana na changamoto za pamoja

Ruto: Afrika ifanye kazi kwa umoja kukabiliana na changamoto za pamoja

0

Rais William Ruto amezitaka nchi za bara la Afrika kufanya kazi pamoja ili kukabiliana na changamoto zake. 

Amesema uongozi wa bara hili lazima uchukue hatua kuelekea mbele na kupigania uhuru wa kiuchumi.

Ruto ameelezea kuwa wakati umewadia kwa Afrika kutumia suluhu kutoka barani humo kusuluhisha matatizo yake.

Alitoa kauli hizo leo Alhamisi mjini Moroni wakati wa maadhimisho ya miaka 48 ya sherehe za siku ya uhuru nchini Comoros.

Rais alitoa wito kwa Afrika kuondoa kizuizi cha mahitaji ya viza ili kuwezesha watu kusafiri kwa njia huru.

Kulingana naye, hatua hiyo ya kijasiri itaongeza biashara baina ya nchi za bara la Afrika na kuchochea ukuaji uchumi.

“Hivyo ndivyo tunavyoweza kuhakikisha ahadi hii ya uhuru inasonga mbele zaidi.”

Rais Ruto alisema Kenya itaondoa mahitaji ya viza kwa raia wa Comoros ili kuimarisha biashara baina ya nchi hizo mbili.

Kadhalika, aliongeza kuwa nchi hizo zitafanya kazi pamoja kuangazia changamoto za pamoja kama vile mabadiliko ya tabia nchi, usalama wa kikanda na maendeleo ya kiuchumi.

“Pamoja, tunaweza tukatumia uwezo wetu wa pamoja kubuni nafasi endelevu za kiuchumi na kukuza ubunifu usiomwacha yeyote nyuma.”

Ruto alimtaka Rais wa Comoros Azali Assoumani kuongoza Umoja wa Afrika, AU kuelekea malengo yanayokidhi mahitaji ya bara la Afrika.

Alitoa wito wa umoja huo kufanyiwa mabadiliko ili kuwezesha AU, taasisi za AU na taasisi maalum kufanya kazi kufikia upeo wa uwezo wake.

Website | + posts