Home Habari Kuu Ruto aapa kuangamiza ufisadi nchini

Ruto aapa kuangamiza ufisadi nchini

0

Rais William Ruto amesema serikali imedhamiria kutokomeza ufisadi humu nchini. 

Amesema mikakati kabambe imeweka kukabiliana na wale wanaokusudia kutumia vibaya fedha za umma.

Rais Ruto amesema serikali inalenga kuhakikisha rasilimali za umma zinatumiwa kufadhili mipango ambayo itabadilisha maisha ya Wakenya.

“Nataka kuwapa ahadi yangu. Katika vita dhidi ya ufisadi, hakutakuwa na majadiliano,” alisema kiongozi wa nchi.

Aliyasema hayo leo Alhamisi katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku ya maendeleo ya siku tatu katika kaunti ya Meru.

Wakati wa ziara hiyo, alizindua miradi kadhaa ya maendeleo katika maeneo bunge ya Buuri, Tigania Magharibi na Tigania Mashariki.

Rais alisema serikali inawekeza katika miradi ya gharama kubwa na uchumi wa dijitali ili kubuni nafasi za ajira na kupanua nafasi za vijana.

Aliongeza kuwa mpango wa nyumba za gharama nafuu umebuni nafasi 130,000 za ajira na vijana wengine 120,000 wanapata kipato kutokana na ajira za dijitali kwa kufanyia kazi mashirika ya kigeni wakiwa nchini Kenya.

Rais Ruto alisema serikali imefanya majadiliano na kupata nafasi za ajira 500,000 kwa vijana walio ughaibuni.

Aliyasema hayo wakati akiwa ameandamana na Mawaziri Mithika Linturi wa Kilimo, Alice Wahome wa Ardhi, Simon Chelugui wa Vyama vya Ushirika, Ezekiel Machogu wa Elimu, Eliud Owalo wa Habari na Mawasiliano na Gavana wa Meru Kawira Mwangaza miongoni mwa viongozi wengine.

 

 

Martin Mwanje & PCS
+ posts