Patrick Aranduh aliapishwa Jumatano kama Kamishna Jenerali mpya wa Magereza katika Ikulu ya Nairobi. Arandu alikula kiapo mbele ya Rais William Ruto katika hafla iliyohudhuriwa na naibu Rais Rigathi Gachagua na katibu mkuu wa idara ya usalama Raymond Omollo.
Rais Ruto alimsifu Arandu kama mtaalamu stadi na alionyesha imani kuwa chini ya uongozi wake, idara ya Magereza itatekeleza shughuli mbalimbali ambazo serikali yake imepanga.
Miongoni mwa mipango ya utawala wa Rais Ruto kwa huduma ya magereza ni utoaji wa makazi bora kwa maafisa hao na kuongeza mishahara yao pamoja na ya maafisa wengine wa polisi.
Kulingana na Rais, maafisa wa magereza pamoja na mashirika mengine ya usalama watakuwa na awamu ya kwanza ya nyongeza ya mishahara kuanzia mwezi huu. Mwaka jana, Rais Ruto aliahidi nyongeza ya asilimia 40 kwa mishahara ya maafisa wa polisi kama ilivyopendekezwa na aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga.
Mnamo Februari mwaka huu, Katibu Mkuu wa Wizara ya usalama Raymond Omollo alithibitisha kwamba nyongeza ya mishahara itaanza Julai mwaka huu, na kutekelezwa hatua kwa hatua katika miaka mitatu ijayo.