Home Michezo Rovanpera atamba siku ya pili ya WRC Safari Rally

Rovanpera atamba siku ya pili ya WRC Safari Rally

0

Bingwa mtetezi wa mashindano ya WRC Kalle Rovanpera amedhihirisha umahiri wake kwa kuibuka mshindi wa siku ya pili ya mashindano ya Safari Rally baada ya kushinda vituo vyote sita vya leo.

Rovanpera akielekezwa na Jonne Haltunen kutoka kampuni ya Toyota Gazoo, aliimarika kutoka nafasi ya nne jana na kutwaa ushindi leo, huku madereva wakistahimili mawe, mabonde na milima katika vituo vya Loldia, Kedong na Geothermal kwenye mzunguko wa asubuhi na wa jioni.

Dereva huyo wa Finland aliongoza siku ya pili ya mashindano kwa jumla ya sekunde 46.4, mbele ya wenzake wa Toyota Katsuta Takamoto na Elyfin Evans waliomaliza katika nafasi za pili na tatu mtawalia.

Mbelgiji Thierry Neuville wa kampuni ya Hyundai aliyeongoza jana amemaliza katika nafasi ya nne dakika 1 na sekunde 41.3 nyuma ya Rovanpera.

Karan Patel akielekezwa na Tauseef Khan wakiendesha gari aina ya Skoda Fabia aliibuka dereva bora wa Kenya na wa 14 kwa jumla, akifuatwa na Carl Tundo na Aakif Virani waliofuatana katika nafasi za 20 na 22 mtaalia.

Hata hivyo, ilikuwa Ijumaa ya nuksi kwa Ott Tanak wa Hyundai aliyelazimika kuyaaga mashindano katika mzunguko wa pili wa kituo cha Geothermal baada ya gari lake kupata ajali, sawia na dereva mwenza Esapeka Lappi.