Home Burudani Rayvanny asema hakuna ugomvi kati yake na Harmonize

Rayvanny asema hakuna ugomvi kati yake na Harmonize

0

Msanii wa muziki nchini Tanzania Rayvanny amesema kwamba hakuna ugomvi kati yake na mwanamuziki mwenza Harmonize.

Vanny boy alikuwa akizungumza katika kikao na wanahabari jijini Dodoma ambapo alielezea kwamba awali kulikuwa na kutoelewana kati yao lakini walisuluhisha.

Alisema awali walikuwa kwenye kampuni moja ya muziki ambapo tofauti za kimakusudi na za mkinzano wa mawazo ziliibuka lakini walizungumza na kuafikiana kama watu wazima.

“Tuliona yaliyotokea kati ya kina BIG na Tupac hatutaki hayo yatokee kwenye nchi yetu.” alisema mmiliki huyo wa kampuni ya muziki ya Next Level.

Rayvanny alisema kwamba huenda wakashirikiana kwenye muziki hivi karibuni na hivyo wafuasi wao watarajie chochote lakini sio kitu ambacho wamepanga kwamba watoe leo au kesho.

Kuhusu tuzo za AEAUSA alizoshinda Harmonize huko Marekani Rayvanny alikuwa na ushauri kwa watu wa taifa la Tanzania hasa baada ya madai kwamba huenda mwanamuziki huyo alinunua tuzo hizo.

Rayvanny alisema watanzania wanafaa kujifundisha kuunga mkono wasanii wao kikamilifu na wala sio kuwapaka tope wanaposhinda ughaibuni.

Harmonize alishinda tuzo ya msanii bora wa mwaka, tuzo ya video bora ya muziki kupitia wimbo wake wa Single Again na tuzo ya mwanamuziki bora wa mtindo wa Bongo Flava. Hafla ya kutuza washindi iliandaliwa Novemba 12, 2023 ambapo Harmonize pia alikuwa mmoja wa watumbuizaji.

Rayvanny na Harmonize walikuwa wamesajiliwa kwenye kampuni ya muziki ya Wasafi inayomilikiwa na Diamond Platnumz kabla ya kuondoka na kila mmoja kuanzisha kampuni yake ya muziki.

Website | + posts