Wizara ya Afya kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani, WHO imeanzisha raundi ya kwanza ya kampeni ya utoaji chanjo ya polio.
Kampeni hiyo inalenga kutoa chanjo milioni 1.8 katika kaunti nne za Garissa, Nairobi, Kiambu na Kajiado.
Katika kaunti ya Garissa, timu za utoaji chanjo zinatarajiwa kuzuru maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo pana wakati wa kampeni hiyo inayowalenga watoto wenye umri wa chini ya miaka 5.
Gavana wa kaunti ya Garissa Nathif Jama aliyekuwa mgeni wa heshima wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo ametoa wito kwa wazazi kutumia fursa hiyo kuhakikisha watoto wao wanachanjwa akiongeza kuwa ugonjwa huo unasababishwa na virusi na kuambukiza kwa kasi na unaathiri hasa watoto.
“Sote tunajua kwamba watoto chini ya umri wa miaka 5 wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa hatari zaidi au kufariki. Na kwa hivyo, nataka kutoa wito kwa wazazi wote kuhakikisha watoto wao wanachanjwa kwa sababu kaunti yetu ni miongoni mwa zile zinazokumbwa na hatari kubwa,” alisema Gavana Jama.
Aliwahakikishia wazazi kuwa chanjo hiyo ni salama.
“Tumehakikishiwa kuwa chanjo ya polio na chanjo zingine ni salama na zitakinga watoto dhidi ya kupooza au kufariki. Kwa hivyo tusihofu juu ya hilo.”
Kampeni hiyo inafuatia mlipuko wa ugonjwa wa polio uliotambuliwa miongoni mwa watoto katika kambi za wakimbizi za Dadaab mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
Inatolewa kwa ushirikiano wa serikali ya Kenya katika viwango vyote na pia mashirika ya WHO, UNICEF na Red Cross.
Dkt. Martins Livinus ambaye ni mwakilishi wa WHO alisema shirika hilo litaendelea kutoa rasilimali muhimu kwa kaunti ya Garissa hasa katika kuimarisha mifumo ambayo itaruhusu kaunti hiyo kuitikia dharura za kiafya kama vile magonjwa ya kipindupindu, polio na mengineyo.
Alitoa wito wa kutolewa kwa huduma za mara kwa mara za utoaji chanjo akiitaja hatua hiyo kama itakayohakikisha wakazi wana kingamaradhi na kuzuia virusi vya polio na magonjwa mengine yanayoweza kuzuiwa kupitia utoaji chanjo.