Home Habari Kuu Rais William Ruto azindua wiki ya uvumbuzi 2023

Rais William Ruto azindua wiki ya uvumbuzi 2023

0

Rais William Ruto leo amezindua wiki ya uvumbuzi ya mwaka 2023 katika taasisi ya mafunzo kuhusu bima, ambayo imetajwa kuwa makala ya Jumuiya ya Madola.

Kulingana na kiongozi wa nchi, Kenya inajenga mfumo wa biashara mpya wenye ushindani mkali ulimwenguni kupitia uondoaji wa vizuizi vya uvumbuzi.

Kuanzishwa kwa mipango ya kutoa motisha, mipango iliyorahisishwa na ufadhili alisema vitavutia wawekezaji zaidi ambao watawekeza fedha kwa biashara hizo mpya na hatimaye kuharakisha kuafikiwa kwa uwezo mkubwa wa kiuchumi wa nchi hii.

“Hatuna budi ila kutambua uvumbuzi kama chombo mwafaka cha kufungua malango ya fursa nyingi,” alisema Rais Ruto.

Aliongeza kwamba vijana hutekeleza jukumu muhimu katika kuwezesha uvumbuzi katika uchumi wa nchi hii na kwamba biashara za uvumbuzi za vijana zilipata ufadhili wa dola milioni 700 mwaka jana na kufanya Kenya kutambuliwa kama eneo bora la uwekezaji barani Afrika.

Kiongozi wa nchi alisema hiyo ndiyo sababu serikali inashabikia mawazo ya kiuvumbuzi kuanzia kwa watoto wachanga kupitia mfumo wa sasa wa elimu, CBC.

Alitaja pia tuzo ya Rais ya uvumbuzi ili kutambua ulio bora zaidi katika sherehe za siku kuu ya Jamhuri.

Makala ya mwaka huu yataangazia uvumbuzi kutoka kaunti zote katika nyanja za uwepo wa chakula na kilimo, mabadiliko ya kidijitali, huduma za afya, burudani na michezo, mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na nishati safi.

Patricia Scotland, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola alihudhuria hafla hiyo ya ufunguzi wa wiki ya uvumbuzi.

Website | + posts