Home Habari Kuu Rais William Ruto afungua rasmi vikao vya bunge la Afrika Mashariki Nairobi

Rais William Ruto afungua rasmi vikao vya bunge la Afrika Mashariki Nairobi

Akihutubia kikao hicho, Rais Ruto alitaja bunge la EALA kuwa kiungo muhimu katika kuhimiza ushirikiano katika kanda na katika maslahi mengine ya eneo hili.

0
Rais William Ruto ahutubia bunge la Afrika Mashariki EALA.

Rais William Ruto leo asubuhi alifungua rasmi kikao cha bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, EALA, katika majengo ya bunge jijini Nairobi, bunge hilo linapoanza rasmi kikao cha tatu cha awamu ya tano.

Akihutubia kikao hicho, Rais Ruto alitaja bunge la EALA kuwa kiungo muhimu katika kuhimiza ushirikiano katika kanda na katika maslahi mengine ya eneo hili.

Bunge la EALA alisema limewezesha kanda hii kutekeleza mpango wa soko la pamoja ambapo watu wa nchi hizo wanavuka mipaka bila vikwazo.

Rais Ruto alisema mkataba huo pia ulitoa fursa ya kuondolewa kwa viwazo visivyo vya ushuru na utekelezaji wa mfumo wa pamoja wa forodha na vituo vya pamoja vya mpakani.

Alisema bunge hilo pia limetoa mkakati wa kukamilishwa kwa mkataba wa biashara huria baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na mashirika ya kikanda ya COMESA na SADC.

Rais Ruto alisifia Jumuiya ya Afrika Mashariki vile vile kama eneo la uwekezaji, nguzo na kitovu cha amani, usalam na biashara barani Afrika.

Kiongozi huyo wa nchi alifika katika majengo ya bunge saa nne asubuhi ambapo alikaribishwa na spika wa bunge la EALA Joseph Ntakirutimana, spika wa bunge la taifa la Kenya Moses Wetangula, mwenzake wa Seneti Amason Kingi na wabunge wa bunge la EALA.

Kikao hicho kinachofanyika katika bunge la seneti kitaendelea kwa majuma matatu.

Website | + posts