Home Kimataifa Rais wa Ukraine asema yuko tayari kwa mazungumzo ya amani na Russia

Rais wa Ukraine asema yuko tayari kwa mazungumzo ya amani na Russia

0
kra

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kwamba yuko tayari kwa mazungumzo ya amani na Russia wakati wowote iwapo Russia itaondoa wanajeshi wake kwenye himaya za Ukraine.

Lakini akizungumza wakati wa kufungwa kwa kongamano kuhusu amani nchini Ukraine lililoandaliwa nchini Switzerland, Zelensky alisema kwamba rais wa Russia Vladimir Putin hawezi kukomesha vita na ni lazima akomeshwe kwa njia yoyote ile iwe ya kijeshi au ya amani.

kra

Zelensky alisema pia kwamba usaidizi wa nchi za magharibi pekee hautoshi katika kushinda vita lakini kongamano hilo limeonyesha kwamba Ukraine inaungwa mkono na mataifa mengi na kamwe haijafifia.

Kufikia mwisho wa kongamano hilo, nchi nyingi zilikuwa zimedhihirisha kwamba zinaunga mkono uadilifu wa himaya ya Ukraine. Viongozi waliohudhuria kongamano hilo walikubaliana na tamko la mwisho la kongamano hilo linaloikosesha Russia kwa kuendelea kwa vita nchini Ukraine.

Hata hivyo kuna nchi ambazo zilikuwa na uwakilishi kwenye kongamano hilo lakini hazikutia saini tamko hilo kama vile India, Afrika Kusini na Saudi Arabia.

Lengo la kongamano hilo lilikuwa kuunda uungwaji mkono kwa mchakato ambao unaweza kukomesha vita vya Russia nchini Ukraine na lilihudhuriwa na viongozi wa nchi zaidi ya 90 na mashirika ya kimataifa.

Russia haikualikwa kwa mkutano huo na China ambayo inaiunga mkono haikuhudhuria, hatua ambayo ilisababisha wengi watilie shaka umuhimu wa kongamano hilo.

Tamko la pamoja la kongamano hilo linaelekeza kwamba Ukraine irejeshe usimamizi wa maeneo yake kama kiwanda cha silaha za nyuklia cha Zaporizhzhia ambacho kwa sasa kinasimamiwa na Russia.

Linataja uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kuwa vita, jina ambalo Urusi imelikataa na linataka mateka wote wa vita hivyo waachiliwe pamoja na watoto waliotekwa nyara na Russia kati ya mapendekezo mengine mengi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here