Home Kimataifa Rais wa Namibia Hage Geingob amefariki

Rais wa Namibia Hage Geingob amefariki

0

Rais wa Namibia Daktari Hage G. Geingob amefariki akiwa na umri wa miaka 82.

Taarifa ya kifo cha kiongozi huyo ilitolewa kupitia mitandao ya kijamii ya afisi ya Rais nchini Namibia.

Kulingana na taarifa hiyo, Geingob, ameaga dunia leo Jumapili Februari 4, 2024 saa kumi alfajiri katika hospitali ya Lady Pohamba jijini Windhoek.

Anasemekana kuaga akiwa amezingirwa na mkewe na wanawe.

Taarifa hiyo imetiwa saini na naibu rais wa Namibia Daktari Nangolo Mbumba ambaye ni kaimu rais wa Namibia kwa sasa.

Jana Mbumba alitoa taarifa kuelezea kwamba rais Hage alikuwa anaugua na kwamba madaktari wake walikuwa wakifanya kila wawezalo kuokoa maisha yake.

Mbumba amemtaja marehemu Hage kuwa kiongozi wa kipekee aliyekuwa mtumishi wa watu, nyota wa ukombozi, mtunzi mkuu wa katiba ya Namibia na nguzo kuu ya nchi hiyo.

“Wakati huu wa majonzi ninaomba wananchi tusalie watulivu serikali inapofanya maandalizi na tangazo kuhusu hilo litatolewa baadaye.” aliandika Mbumba.

Rais huyo wa muda ameitisha mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri ili kufanya mipango inayohitajika.

Hage Gottfried Geingob ni rais wa tatu wa taifa la Namibia na alianza kuhudumu katika wadhifa huo Machi 2015 hadi kifo chake hii leo.

Alihudumu kama waziri mkuu wa kwanza wa Namibia kati ya mwaka 1990 na 2002, na kati ya mwaka 2012 na 2015.

Alikuwa waziri wa biashara na viwanda mwaka 2008 hadi 2012 na amekuwa pia kiongozi wa chama tawala cha SWAPO tangu Novemba 2017 hadi leo.

Ameacha mke Monica Kalondo Geingos na watoto watatu.

Website | + posts