Home Habari Kuu Rais wa Iran Ebrahim Raisi awasili nchini Kenya

Rais wa Iran Ebrahim Raisi awasili nchini Kenya

Raisi yuko katika ziara ya siku tatu barani Afrika, huku akitarajiwa kuzuru Kenya, Uganda, na Zimbabwe.

0
Rais wa Iran Ebrahim Raisi, awasili nchini Kenya.

Rais wa Iran Ebrahim Raisi amewasili nchini Kenya. Kiongozi huyo wa Jamuhuri ya Iran alilakiwa na Waziri wa Mambo ya Nje Dkt. Alfred Mutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa  Jomo Kenyatta. 

Raisi alielekea katika Ikulu ya Nairobi, alikolakiwa na mwenyeji wake Rais William Ruto na kisha kukagua gwaride la heshima.

Baada ya sherehe hiyo fupi, viongozi hao wawili wanatarajiwa kushiriki mazungumzo ya pande mbili, yanayolenga kuimarsha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Baadaye kiongozi huyo wa Iran ataweka shada la maua katika kaburi la hayati mzee Jomo Kenyatta.

Ziara hiyo ya Raisi barani Afrika na ambayo ni ya kwanza kwa kiongozi wa Iran katika muda wa miaka 11, ilicheleweshwa kwa siku moja kutoa fursa ya kukamilishwa kwa mikataba muhimu ya makubaliano kati ya Kenya na Iran.

Raisi alitarajiwa kuandaa mkutano wa pamoja wa wanahabari na Rais William Ruto jana Jumanne, lakini mkutano huo ukafutiliwa mbali.

Raisi yuko katika ziara ya siku tatu barani Afrika huku akitarajiwa kuzuru Kenya, Uganda, na Zimbabwe.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here