Home Kimataifa Rais Samia kuongoza mazishi ya Lowassa

Rais Samia kuongoza mazishi ya Lowassa

0
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Edward Lowassa.

Mwili wa marehemu Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Edward Lowassa utazikwa Jumamosi, Februari 17, 2024 nyumbani kwake katika wilaya ya Monduli, eneo la Arusha.

Waziri Mkuu wa sasa Kassim Majaliwa amesema kwamba kiongozi wa taifa hilo Rais Samia Suluhu Hassan ataongoza hafla hiyo ya mazishi.

Awali, Rais Samia alitangaza kipindi cha maombolezi ya kitaifa cha muda wa siku tano kuanzia Februari 10, 2024 na katika muda huo wote, bendera zilifaa kupeperushwa nusu mlingoti.

Lowassa aliandaliwa mazishi ya kitaifa katika uwanja wa Karimjee jijini Dar es Salam, hafla iliyoongozwa na Naibu Rais wa Tanzania Dkt. Phillip Mpango.

Wakati wa hafla hiyo, Dkt. Mpango alimtaja marehemu Lowassa kuwa mfanyakazi wa umma aliyejitolea katika nyadhifa zote ambazo aliwahi kushikilia.

Jana Jumatano, mwili wa Lowassa ulipelekwa katika kanisa la kiluteri la Azania Front kwa ibada ya wafu iliyohudhuriwa na wananchi wengi.

Leo Alhamisi, mwili huo unasafirishwa kwa ndege hadi Arusha ambapo raia na viongozi mbalimbali watapata fursa ya kuona na kutoa heshima za mwisho katika uwanja wa michezo wa Sheikh Amri Abeid Kaluta.

Lowassa ambaye aliwahi kuwania urais aliaga dunia Jumamosi Februari 10, 2024 akipokea matibabu katika hospitali ya matibabu ya moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam.

Website | + posts