Home Kimataifa Rais Samia amkabidhi Janeth Maghufuli nyumba

Rais Samia amkabidhi Janeth Maghufuli nyumba

0

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amemkabidhi rasmi nyumba ya makazi mjane wa Rais wa zamani John Pombe Maghufuli Janeth Maghufuli.

Hafla ya kukabidhi nyumba hiyo rasmi iliandaliwa Jumapili Novemba 5, 2023.

Nyumba hiyo ambayo iko katika wilaya ya Kinondoni, mkoa wa Dar es Salaam, ilijengwa na serikali ya muungano wa Tanzania kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza wakati wa kumkabidhi mama Janeth Nyumba hiyo, Rais Samia alimrejelea kama ndugu huku akimwomba apokee nyumba hiyo kwa moyo mkunjufu.

Rais alikiri kujawa na hisia mseto alipomkumbuka Maghufuli ambaye alimrejelea kuwa mlezi wake kisiasa.

Mama Janeth naye alishukuru kwa nyumba hiyo akisema kwamba ni tendo lililotukuka na alama isiyofutika katika mioyo ya watu wa familia ya marehemu Maghufuli kwani itakuwa makazi yao ya kudumu.

Alisema zawadi pekee ambayo anaweza kumpa Rais Samia ni kumwombea mema kwa Mola ili aendelee vyema kwenye kazi zake.

Wawili hao walikumbatiana huku Janeth akibubujikwa na machozi, Rais alikata utepe wa kuingia kwenye nyumba hiyo na kumkabidhi Janeth mwigo wa ufunguo na wakaingia ndani.

Nyumba hiyo ilionekana kuwa na samani tayari na ina picha kubwa ya hayati Maghufuli kwenye ukuta.

Website | + posts