Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametangaza mabadiliko madogo katika baraza la mawaziri pamoja na teuzi kadhaa za afisi muhimu serikalini.
Katika mabadiliko hayo, Ummy Mwalimu ambaye amehudumu kama waziri wa afya kwa muda mrefu ameodnolewa wadhifani na mahala pake kuchukuliwa na Jenista Mhagama.
Awali Mhagama alihudumu kama waziri katika afisi ya waziri mkuu aliyehusika na masuala ya sera, bunge na uratibu.
Profesa Palamagamba Kabudi amerejea kwenye baraza la mawaziri katika wadhifa aliohudumu awali wa waziri wa masuala ya katiba ba sheria huku William Lukuvi akichukua wadhifa wa awali wa Mhagama katika afisi ya waziri mkuu.
Balozi Pindi Chana ameteuliwa waziri wa maliasili na utalii wadhifa uliokuwa ukishikiliwa na Angellah Jasmine Kairuki, ambaye ameteuliwa kuwa mshauri wa Rais.
Hamza Johari ambaye amekuwa akihudumu kama mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya usafiri wa angani nchini Tanzania ameteuliwa kuwa mwanasheria mkuu.
Samwel Maneno ameteuliwa naibu mwanasheria mkuu baada ya kuhudumu kama mshauri wa Rais katika masuala ya kisheria. Wadhifa anaochukua ulikuwa ukishikiliwa na balozi Profesa Kennedy Gastorn ambaye sasa amefanywa mshauri wa Rais katika masuala ya sheria na mikataba.
Rais Samia amemteua Daktari Ally Saleh Possi kama wakili wa serikali. Kabla ya uteuzi huo Possi alikuwa naibu katibu wa kudumu katika wizara ya uchukuzi.
Walioteuliwa wanaapishwa leo Agosti 15, 2024 jijini Dar es Salaam.