Home Habari Kuu Rais Ruto: Yaacheni mashirika ya kutoa misaada yafanye kazi kwa njia huru

Rais Ruto: Yaacheni mashirika ya kutoa misaada yafanye kazi kwa njia huru

0
Rais Ruto alipokutana na Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi.
Rais Ruto alipokutana na Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi.

Rais William Ruto amezitaka pande zinazozozana nchini Sudan kuruhusu mashirika ya kutoa misaada ya binadamu kuendesha shughuli zao kwa njia huru.

Rais Ruto amesema mashirika hayo yanasaidia kuepusha mateso yaliyosababishwa na mzozo huo na kazi zao zinapaswa kuendelea bila kuzuiwa.

Aliyasema hayo alipokutana na Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi aliyemtaarifu juu ya hali ya kibinadamu na janga la wakimbizi nchini Sudan.

Grandi alimuambia Rais Ruto, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kundi la Nchi Nne la mpango wa IGAD kuhusu upatikanaji wa amani nchini Sudan, kwamba mapigano yameongezeka na idadi ya wakimbizi wanaotoroka vita inatarajiwa kufikia milioni mbili.

“Idadi kubwa ya wakimbizi kwenye mipaka ya Misri na Chad imesababisha mateso mengi,” alisema Grandi.

“Kitu kinachohuzunisha zaidi ni kwamba wafanyakazi wa kutoa misaada hawaheshimiwi na ofisi ya UNHCR mjini Khartoum imeharibiwa.”

Kama mwenyekiti wa Kundi la Nchi Nne za IGAD, Rais Ruto alisema wanafanya kazi kumaliza mzozo huo.

Nchi hizo nne ni pamoja na Kenya, Sudan Kusini, Ethiopia na Djibouti.

Rais Ruto alisema Baraza la Mawaziri wa kundi hilo lilikutana jana Jumatatu chini ya uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Alfred Mutua.

Grandi alimtaarifu Rais kwamba UNHCR imepokea mchango mkubwa kwa jitihada zake za kibinadamu baada ya wito wa uchangishaji fedha kusababisha kutolewa kwa dola bilioni  1.5 jana Jumatatu.

Alielezea kuwa shirika hilo linatafuta dola bilioni tatu.

Rais Ruto alilipongeza uchangishaji fedha huo na kumshukuru Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwa uongozi wake bora.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here