Home Habari Kuu Rais Ruto: Uwezo wa walinzi wa misitu umeboreshwa

Rais Ruto: Uwezo wa walinzi wa misitu umeboreshwa

0

Rais William Ruto amesema kwamba uwezo wa walinzi wa misitu umeboreshwa na serikali ili waweze kulinda misitu ifaavyo.

Aliongeza kusema kwamba serikali imewekeza katika teknolojia itakayoboresha doria, ukusanyaji data na usimamizi wa misitu unaoongozwa na ushahidi.

Kiongozi wa nchi ambaye alikuwa akizungumza huko Gilgil katika kaunti ya Nakuru kwenye hafla ya kufuzu kwa walinzi wa misitu alitaja uboreshaji wa mafunzo kwa walinzi hao na vifaa vya kazi ili kuwiana na mahitaji ya majukumu yao.

Alielezea kwamba lengo ni kukabiliana na ukataji haramu wa miti, uchomaji makaa na njia nyingine za uharibifu wa misitu.

Rais alitambua kwamba mabadiliko ya tabianchi ambayo huweka wakenya katika mazingira magumu yanatokana na hulka mbaya ya binadamu kama vile kuharibu misitu.

Changamoto ya kiongozi wa nchi kwa walinzi hao wa misitu ni kwamba waongoze utekelezaji wa mpango wa kitaifa wa kurejesha mandhari na mfumo ikolojia ili kuafikia mpango wake wa upanzi wa miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032.

Rais alisema mpango wa maendeleo nchini unategemea mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kwamba Kenya inatambulika Afrika na ulimwenguni kwa mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Waziri wa Mazingira na Misitu Soipan Tuya, magavana Susan Kihika wa Nakuru na Andrew Mwadime wa Taita Taveta, wabunge wakiongozwa na Martha Wangari wa eneo hilo, wawakilishi wadi na viongozi wengine walihudhuria hafla hiyo.

Website | + posts