Serikali inaongeza uwekezaji katika unyunyiziaji mashamba maji, ili kuimarisha uwezo wa taifa hili wa uzalishaji chakula, hayo ni kwa mujibu wa Rais William Ruto.
Rais Ruto alisema unyunyizaji mashamba maji utasaidia taifa hili kuongeza kiwango cha ardhi ya kilimo na kusitisha utegemeaji wa mvua kwa shughuli za kilimo.
Alisema uwekezaji wa shilingi bilioni 60 katika miradi ya maji, utasaidia kupunguza uagizaji chakula ambacho kinaweza kuzwa hapa nchini.
“Kila mwaka, taifa hili hutumia shilingi bilioni 500 kuagiza chakula kinachokuzwa na wakulima kutoka mataifa mengine. Tunataka fedha hizi ziwaendee wakulima wetu,” alisema Rais.
Rais aliyasema hayo katika eneo la Gatundu kaunti ya Kiambu, alikozindua awamu ya kwanza ya mradi wa unyunyiziaji mashamba maji wa Rwabura, utakaowahudumia wakulima 5,000 na kutoa nafasi 25,000 za ajira.
Awali kiongozi huyo wa taifa alizindua mradi wa usambazaji maji wa kijamii wa Mathira, ambao utawafaidi watu 25,000.
Walioandamana na Rais ni pamoja na naibu Rais Rigathi Gachagua, Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi, wabunge wakiongozwa na kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichungw’ah na wawakilishi wadi kadhaa.