Home Habari Kuu Rais Ruto: Tunapaswa kukomboa ugatuzi dhidi ya ufisadi

Rais Ruto: Tunapaswa kukomboa ugatuzi dhidi ya ufisadi

0
Rais William Ruto.

Rais William Ruto ameonya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya maafisa watakaofuja rasilimali za umma.

Alisema kuwa, huku serikali ya litaifa ikiendelea kuunga mkono ugatuzi katika kuboresha maisha ya wakenya, hatakuwa na huruma kwa wale wanaofuja fedha za umma.

Kiongozi wa taifa alitoa wito wa kutumiwa vyema kwa rasilimali za umma ili kutoa miradi zaidi ya maendeleo itakayoimarisha maisha ya wakenya wa kawaida.

“Haikuwa lengo la watu wa Kenya kugatua ufisadi, usimamizi mbaya na maadili yasiyofaa katika kaunti,” alisema Rais Ruto.

Rais alisikitika kuwa kaunti nyingi zimeghubikwa na uporaji wa mali huku kila mmoja kutoka kwa gavana hadi maafisa wa chini zaidi katika kaunti wakihusika katika uovu huo badala ya kutoa huduma.

“Wakenya wengi wasio na hatia wanapokea huduma duni au kutengwa kutokana na uhalifu uliogatuliwa,” alisikitika Rais.

Aidha kiongozi wa taifa aliweka bayana kuwa ufisadi hautasazwa katika viwango vyote vya serikali.

“Licha ya cheo, wadhifa au hadhi, yeyote atakayehusishwa na ufujaji wa fedha, katika serikali ya kitaifa au ya kaunti, lazima awajibikie matendo yake kikamilifu,” alisema Rais Ruto.

Alizitaka asasi husika kuharakisha kushughulikia kesi za ufisadi zilizoko katika kaunti nyingi.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here