Home Habari Kuu Rais Ruto: Sitakubali Wakenya kufariki kwa sababu ya maandamano

Rais Ruto: Sitakubali Wakenya kufariki kwa sababu ya maandamano

0

Rais William Ruto amewahakikishia Wakenya kuwepo kwa amani kote nchini kesho Jumatano. 

Muungano wa Azimio umepanga kufanya maandamano kote nchini Kesho Jumatano.

“Kesho kutakuwa na amani Kenya. Walifanya maandamano Ijumaa, Wakenya wakapoteza maisha yao. Sitakubali Mkenya yeyote kupoteza maisha yake ili mtu mwingine atimize maono yake ya kisiasa. Hilo halitafanyika,” alisema Rais Ruto wakati wa hafla ya utoaji hatimiliki za ardhi katika eneo la Embakasi.

“Mimi nataka niwaambia hawa watu wa maandamano, wachaneni na vijana wa Kenya. Sisi tunawajua, na tunajua mbinu zenu na zitaanguka vile zilianguka mbeleni na vile huwa zinaanguka kila siku. Msipoteze wakati,”

Kauli sawia zilitolewa na Naibu Rais Rigathi Gachagua ambaye alionya kuwa yeyote atakayehusika katika visa vya uvunjaji wa sheria wakati wa maandamano ya Azimio atakabiliwa vikali kisheria.

Gachagua pia alikanusha madai kuwa Waziri wa Usalama wa Taifa Prof. Kithure Kindiki wakati akizungumza katika eneo la Isebania aliwataka maafisa wa polisi kutowakabili vikali wanaovunja sheria na kutotumia nguvu.

“Maafisa wetu wa usalama wanapaswa kutumia sheria na kuwakamata wanaovunja sheria bila kujali vyeo vyao,” alisema Gachagua aliyevishutumu vyombo vya habari kwa kumnukuu Kindiki visivyo.

“Wewe ukienda kutoa fujo kesho, utakamatwa. Serikali yetu haiwezi ikakubali mtu atoke kwake, akuje kuchafua amani, kuharibu mali ya raia na kuzuia watu kufanya biashara.”

Muungano wa Azimio umeitisha maandamano ya kupinga kupanda kwa gharama ya maisha na utekelezaji wa sheria ya fedha ya mwaka 2023.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here