Home Habari Kuu Rais Ruto: Serikali itashirikiana na Kanisa kuboresha maisha ya wakenya

Rais Ruto: Serikali itashirikiana na Kanisa kuboresha maisha ya wakenya

Rais alisema serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa katika kuanzisha miradi ya maendeleo inayolenga kuwawezesha wananchi.

0
Rais William Ruto.

Serikali na mashirika ya kidini, yana jukumu la ushirikiano katika kukabiliana na matatizo ya kijamii na kuwezesha jamii kiuchumi, Rais William Ruto amesema.

Rais alisema serikali na Kanisa, kwa hivyo, zitaendelea kufanya kazi pamoja ili kuboresha hali ya maisha ya Wakenya.

Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa 24 wa kanisa la PCEA, katika Kanisa la St Andrews jijini Nairobi, Rais Ruto alipongeza jukumu lililotekelezwa na makanisa katika maendeleo ya elimu na afya miongoni mwa mengine.

“Tunathamini nafasi ya kanisa katika masuala ya elimu, afya na kujenga uelewa juu ya masuala mbalimbali,” alisema.

Rais alisema serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa katika kuanzisha miradi ya maendeleo inayolenga kuwawezesha wananchi.

Alitoa wito kwa viongozi wa Kanisa kusaidia serikali kutokomeza pombe haramu, dawa za kulevya na changamoto za ukosefu wa usalama zinazotokana na ujambazi na wizi wa ng’ombe.

Alisikitika kwamba familia nyingi zimeathiriwa na vitisho vya pombe haramu na dawa za kulevya, haswa kwa sababu vijana wengi wamekuwa waraibu wa dawa hizo.

Rais amekuwa akisisitiza kuwa hakuna juhudi zozote zitakaaitishwa katika kutokomeza maovu hayo mawili.

Alikiri kwamba ukosefu wa ajira umechangia pakubwa unywaji pombe na utumizi wa dawa za kulevya, akiongeza kuwa akili isiyo na kazi ni warsha ya shetani.

“Hii ndiyo sababu tuna mpango thabiti na wa makusudi, kupitia mpango wa nyumba za bei nafuu na uchumi wa kidijitali, kuunda nafasi za kazi kwa watu wetu. Kwa hakika, sasa tuna vijana 140,000 wanaofanya kazi katika mpango wa makazi kote nchini,” alisema.

Rais alidokeza kuwa serikali ilikuwa ikikamilisha makubaliano ya kazi baina mataifa 19 ambayo yatasaidia watu wengi zaidi kupata kazi nje ya nchi au kufanya kazi bila kulazimika kuenda ofisini kwa mashirika ya kigeni kutoka Kenya.