Home Habari Kuu Rais Ruto kufanya ziara ya siku mbili Msumbiji

Rais Ruto kufanya ziara ya siku mbili Msumbiji

0

Rais William Ruto leo Alhamisi ataelekea nchini Msumbiji kwa ziara ya siku mbili. 

Hii ni kwa mujibu wa msemaji wa Ikulu ya Nairobi Hussein Mohamed.

Mohamed anasema wakati wa ziara hiyo, Ruto atafanya majadiliano na mwenyeji wake ambaye ni Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi kwa lengo la kuimarisha na kupanua uhusiano wa pande mbili kati ya nchi hizo.

Kiini cha mazungumzo kati yao kitakuwa uangaziaji wa sekta muhimu kama vile uchumi wa bahari na uvuvi, biashara, ulinzi, kilimo, nishati, uchukuzi na ukuzaji uwezo.

Marais Ruto na Nyusi pia watashuhudia kutiwa saini kwa makubaliano 8 ya ushirikiano na hivyo kuimarisha dhamira yao ya pamoja ya ushirikiano kati ya Kenya na Msumbiji.

Aidha ziara hiyo itaongeza ari ya kuandaliwa kwa kongamano la biashara kati ya Kenya na Msumbiji ambalo litatafuta namna ya kunufaika ipasavyo kutokana na fursa za kiuchumi za pande mbili mbali na kuadhimisha uzinduzi wa Kamati ya Pamoja ya Biashara, JTC kati ya nchi hizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here