Home Habari Kuu Rais Ruto kufanya ziara rasmi Ghana na Guinea-Bissau

Rais Ruto kufanya ziara rasmi Ghana na Guinea-Bissau

Akiwa nchini Ghana, kiongozi wa taifa atasisitiza umuhimu wa juhudi za ushirikiano ili kuimarisha na kuunganisha utawala wa kidemokrasia barani Afrika.

0
Rais William Ruto afanya ziara ya kiserikali nchini Ghana na Guinea-Bissau.

Rais William Ruto ataondoka hapa nchini leo Jumanne kwa ziara ya kiserikali nchini Ghana, ikifuatiwa na ziara rasmi nchini Guinea-Bissau.

Katika ziara hizo, Rais Ruto atafanya mazungumzo na marais Nana Akufo-Addo wa Ghana na Umaro Sissoco Embaló wa Guinea-Bissau, kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, ushirikiano wa kibiashara na kihistoria kati ya Kenya na mataifa hayo mawili ya Afrika Magharibi.

Akiwa nchini Ghana, kiongozi wa taifa atasisitiza umuhimu wa juhudi za ushirikiano ili kuimarisha na kuunganisha utawala wa kidemokrasia barani Afrika.

Pia atazuru makao makuu ya eneo la biashara huru barani Afrika (AfCFTA) Jijini Accra, akilenga kuimarisha uuzaji wa bidhaa za majani chai na ngozi kutoka Kenya nchini Ghana.

“Juhudi hizi zitaungwa mkono na mikataba ya maelewano kati ya mashirika ya sekta za kibinafsi na umma, inayolenga kuboresha biashara kati ya Kenya na Ghana chini ya eneo la biashara huru la bara Afrika (AfCFTA),” alisema msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed kupitia kwa taarifa.

Rais Ruto pia atahutubia kongamano la biashara kati ya Ghana na Kenya ili kutafuta fursa za uwekezaji na biashara katika sekta mbalimbali.

Na akiwa nchini Guinea-Bissau, Rais Ruto ataimarisha uhusiano wa kibiashara pamoja na kutafuta fursa mpya za ushirikiano, kupitia eneo la biashara huru barani Afrika.

“Hii itajumuisha kuimarisha sekta ya kibinafsi kushiriki katika kilimo, utengenezaji bidhaa na teknolojia miongoni mwa sekta zingine,” ilisema taarifa hiyo.